Jamaa aliyechomwa nyeti zake kwa maji moto na mkewe asema bado anampenda

Mwanamume huyo alisema hawezi kushiriki mapenzi na mkwe kwani hospitalini ilibidi nyeti zake zikatwe na kutupwa kutokana na kuharibika kwa kuunguzwa na maji moto.

Muhtasari

• "Tunaishi na mke wangu kama kida dada wawili kwa sababu hatuwezi fanya mapenzi.” alisema.

• "Hospitalini nilihudumiwa, ikabidi uume wangu kukatwa na kutupwa kabla ya kuruhusiwa kurudi nyumbani,” Ntezimana alisema.

Mwanaume aliyechomwa kwa maji moto na mkewe ,amsamehe.
Mwanaume aliyechomwa kwa maji moto na mkewe ,amsamehe.
Image: Screengrab//YouTube

Mwanamume mmoja amewashangaza wengi baada ya kuhadithia jinsi mke wake alimmwagia maji ya moto na kumchoma vibaya mwili mzima hadi kupelekea kupoteza nyeti zake, lakini bado anasisitiza kwamba mapenzi yake kwa mkewe hayawezi yumbishwa.

Ntezimana Jean Baptiste alisumilia kisa chake katika chanelo moja ya mitandaoni jinsi mambo yalivyomwendea mrama siku moja alipotoka kazini na kumpata mkewe amenuna na kuanzisha timbwiri la kufa mtu.

Akionesha majeraha ya kuunguzwa kwa maji moto mwilini, kote kunakoonekana na kusikoonekana, Ntezimana alisema kuwa hakutarajia tukio hilo lingemtokea hadi kupoteza nyeti zake ambapo sasa hawezi tena kushiriki tendo la ndoa.

“Nilikuja nyumbani kutoka kwa baa na nilipofika nyumbani, mke wangu alikuwa amenuna wakati nilimsalimia. Alikuwa anaongea kwa shari na kisha akanivuta shingoni baada ya kunikaba kwenye koo. Mzozo ulitokea kidogo kisha mimi nikaingia kitandani nikidhani yameisha. Nilitarajia asubuhi iliyofuata tungeyasuluhisha, kumbe sikujua kesho yenyewe haikuwa imehakikishwa,” alikumbuka.

Alipojilaza kitandani akidhani kila kitu kilikuwa sawa, mkewe alitimba jikoni na kuchemsha maji ambapo alimvizia kwenye malazi yake na kummwagia hivyo kumuunguza sehemu kubwa ya mwili wake.

“Nililala na kuamka kwa uchungu wa kuunguzwa na maji moto kwenye uume wangu, mwili mzima na hata hapa kwenye mikono (akionesha). Hospitalini nilihudumiwa, ikabidi uume wangu kukatwa na kutupwa kabla ya kuruhusiwa kurudi nyumbani,” Ntezimana alisema.

Ntezimana ambaye hadi sasa hajapata kupona vizuri bado anajikongoja kwa magongo lakini anasema mapenzi yake kwa mkewe bado hayawezi kubadilika.

“Ninaishi kwa uchungu sana, mimi si mwanaume tena maana nilishapoteza uume wangu. Niko na mke na watoto wawili na tunaishi pamoja. Tunaishi na mke wangu kama kida dada wawili kwa sababu hatuwezi fanya mapenzi.”

Kwa upande wa mkewe, anakiri kwamba waligombana lakini hakuhusika katika kumuunguza mumewe kwa maji moto, jambo ambalo hata hivyo mumewe analipinga vikali akisema kuwa hakuna mtu mwingine angeingia kwenye chumba chao cha malazi naiwapo ni mtu mwingine basi mkewe angefanya hima hata kupiga kamsa kuitisha usaidizi.

“Nilikuwa nachemsha maji ya ugali wakati niliyaacha na kuelekea dukani kununua unga, niliporudi nilipata ameunguzwa na amepelekwa hospitali,” mkewe alisema.

Wawili hao wameishi hivyo na simulizi kinzani kuhusu kilichotokea huku mume akisisitiza ni mkewe alifanya hivyo na mke akikanusha.

Waliamua kuishi pamoja kwa ajili ya watoto katika kile mume alisema kuwa bado anampenda kupita maelezo mkewe.