Hela au Sera -Wakenya tuache siasa za hela tuzingatie sera

Muhtasari

• Tumewaona wanasiasa wengi wakimwaga hela katika maeneo mengi humu nchini.

• Wengi hatujui ni sera zipi zilichochea uamuzi wetu kuwapigia kura watu fulani, lakini tunalofahamu ni pesa ngapi kila mmoja alikuwa akigawa.

Foleni ndefu katika shule ya msingi ya Kinango wananchi wakisubiri mchakato wa upigaji kura kuanza, AGOSTI 9/2022.
Foleni ndefu katika shule ya msingi ya Kinango wananchi wakisubiri mchakato wa upigaji kura kuanza, AGOSTI 9/2022.

Miaka nenda miaka rudi, tumekuwa tukilisukuma hili gurudumu la uongozi katika nchi ya Kenya.

Uchaguzi umefanyika na sasa tuko mkondo wa mwisho, lakini humu nchini mambo yamesalia vile vile, kwani kila yanapobadilika ndipo yanasalia vile,  Kwa  kimombo the more things change , the more they remain the same .

Kifo cha afisa wa tume ya uchaguzi siku chache zilizopita, sio jambo geni hapa Kenya wakati wa uchaguzj. Je kama wakenya tumeridhika na yale tumeshuhudia , kutoka kwa rabsha ndani ya ukumbi wa Bomas huku wengi wa makamishna wa IEBC wakijitenga na matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na mwenyekiti wa tume Wafula Chebukati.

Kwa muda wa siku kadhaa vyombo vya habari viliacha kutuonyesha yanayojiri . Wakenya tuliachwa kwa mataa huku kila mmoja wetu akijitwika jukumu la kuhesabu kura, wengi hata hivyo walilemewa kuhesabu kura milioni 14 . Mengi yamejiri na kuna mengi ambayo bado wengi wetu yametuacha na maswali mengi kuliko majibu.

Katika uchaguzi huu kuna mengi nimejionea ambayo tunafaa kurekebisha kama Wakenya. Tumewaona wanasiasa wengi wakimwaga hela katika maeneo mengi humu nchini. Zikawa siasa za hela na sio sera . Wengi wetu hata hatujui ni sera zipi zilichochea uamuzi wetu kuwapigia kura watu fulani, lakini tunalofahamu ni pesa ngapi kila mmoja alikuwa akigawa.Tunakumbuka vyema fulani alikuwa akigawa hamsini hamsini na mwengine mia mia.

Tukawafanya wanasiasa kuanza kuonyesha ubabe wao nani angegawa pesa nyingi zaidi ya mwingine.Tutabaki tukijikuna vichwa, kwani hela hizi zitarejeshwa aje?. Wanasaisa walichukuwa mikopo na hata kunadi mali zao kufadhili kampeini zao.

Tukizangatia mshahara wa mwanasiasa katika kipindi cha miaka mitano halafu tulinganishe na kiasi cha fedha walichotumia, bila shaka hawawezi  kurejesha pesa hizo kwa mishahara yao pekee. Wakenya wenzangu mjiulize swali, Je watajilia vipi pesa hizi. 

Kura humu nchini Kenya huambatana na hisi kali, kwanini haswa?, tunafaa kujiuliza maswali kama haya . Je! hawa wanasiasa wote wana nia ya kutuwakilisha na kututendea mema, na kwanini mtu awekeze kiasi kikubwa cha fedha kukuwakilisha wewe?. Sisi ndio wakulaumiwa kwa hali hii.

Umefika wakati mwanasiasa hawezi wasalimia watu wake mkono mtupu . Mheshimiwa wacha kitu boma itulie . Mheshimiwa hawezi hudhuria misa bila mchango wa kanisa kujitokeza. Wengi sasa tunaangalia mwanasiasa kwenye mizani ya michango wanayotoa na kina cha mifuko yao.  Tunajutia na kusaga meno tukijiuliza kwanini hatuna maendeleo tunayotaka .

Tusipo badalisha dhana yetu ya kujihamasisha kuhusu uchaguzi bora tutaendelea kusaga meno. Gharama ya maisha itazidi kupanda na sisi ndio  wakulaumu .

 Wakenya tuachane na siasa za hela na tuzingatie sera.