(+video) Mchungaji wa Zimbabwe aliyetabiri ushindi wa rais mteule Ruto

"Mungu alinipa ufunuo kwamba ni Ruto" - Mchungaji Uebert Angel alisema.

Muhtasari

• “Hii ilikuwa ni vita kati ya jana (Uhuru) na kesho (Ruto) na mnajua kesho siku zote inashinda,” mchungaji huyo alisema.

Wiki kadhaa kuelekea uchaguzi mkuu, palizuka video ya mhubiri mmoja kwa jina Uebert Angel akisema kwamba Mungu amempa ufunuo kubashiri matokeo ya uchaguzi wa Keya ambao ulifanyika nchini Agosti 9.

Mchungaji Angel Uebert anaonekana kwenye video akisema kwamba Mungu alimpa ufunuo wa kusema kwamba naibu rais anayeondoka William Ruto ndiye atakayeibuka kidedea dhidi ya mshindani wake mkuu Raila Odinga.

Katika video nyingine sasa, mchungaji huyo ameibuka akisema kwamba Mungu alimuambia rais anayeondoka Uhuru Kenyatta hatoweza kumsimamisha Ruto katika mbio zake za kuelekea ikulu ya Nairobi.

“Mungu aliniambia kwamba Uhuru hawezi kumzuia Ruto. Kulikuwepo muda wa Uhuru na sasa kuna muda wa Ruto, hata kama utapinga au kufanya kitu chochote, Ruto ni Ruto, Mungu anasema kwamba ni muda wa Ruto,” mchungaji huyo anaonekana akihubiri katika video aliyoipakia Instagram yake.

Uebert Angel anazidi kuwataka waumini wote kutamka jina la Ruto na pia kusema kwamba uchaguzi huo ulikuwa ni vita kati ya yaliyopita ambayo ni rais Kenyatta na kesho ambayo ni rais mteule William Ruto.

“Hii ilikuwa ni vita kati ya jana (Uhuru) na kesho (Ruto) na mnajua kesho siku zote inashinda,” mchungaji huyo alisema.

Ruto alikabidhiwa cheti cha ushindi na mwenyekiti wa tume ya IEBC mapema wiki hii baada ya kinyang’anyiro kikali baina yake na Raila Odinga aliyekuwa akiwania urais kwa mara ya tano na kumshinda na mchungaji huyo sasa ameibuka kujidai kwamba ni kweli jinsi alivyowaambia wangu unabii wake lakini hawakumuamini.