• Karen Nyamu alisema Ruto alishinda hali ya hewa ikabadilika huku akisema kwamba rais huyo mteule atawaunganisha wakenya wote.
Wakili Karen Nyamu ambaye ni mmoja kati ya watetezi wakali wa sera za naibu wa rais anayeondoka William Ruto anadai kwamba tangu Ruto atangazwe na IEBC kama rais mteule, kila kitu kimebadilika na hata hali ya hewa nchini imebadilika kwa Wakenya kutoka matabaka yote ya maisha.
Nyamu kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii aliandika kwamba Upepo wa matumaini na matarajio kwa Wakenya wote ndicho kinachohakiniza katika janibu zote nchini tangu Ruto kupokezwa cheti cha ushindi wa urais.
“Ni mimi tu ama hali ya hewa nchini imebadilika? Upepo wa matumaini na matarajio kwa Wakenya wa matabaka mbalimbali! Ni mapambazuko mapya kwa KENYA. Yaliyopita si ndwele. Nina hakika kwamba Rais wetu William S Ruto atatuunganisha sisi sote kama Wakenya, bila kujali kabila na itikadi za kisiasa,” Nyamu alidhihirisha matumaini yake kwa rais mpya mtarajiwa.
Mwanasiasa huyo mchanga awali alikuwa ameweka wazi azma yake ya kutaka kuwania kama seneta wa Nairobi kupitia chama cha UDA ila baada ya mashauriano ya kina na uongozi wa chama, alisema kwamba alishauriwa kuzima kwa muda azma hiyo yake na tikiti hiyo ikakabidhiwa kwa Askofu Margret Wanjiru ambaye alimenyana na Edwin Sifuna wa ODM na kuibuka wa pili kwa kura zaidi ya laki tano.
Nyamu amekuwa akionekana katika mikutano na misafara ya kampeni ya William Ruto akimpigia debe na sasa anasema kwamab serikali yao itakuwa moja ya kupigiwa mfano si tu katika bara la Afrika bali kote duniani.