Watekaji nyara waliodanganya mtoto wa miaka 6 wangemnunulia viazi ili aanguke kwenye mtego wakamatwa Mathare

Muhtasari

•Kulingana na DCI, wawili hao walimteka nyara Collins Orina wakati alikuwa anacheza na rafiki yake nje ya kanisa  la Kware SDA. 

•Mhasiriwa alikubali kumfuata jamaa yule na wakatoweka  ila rafiki yake akarejea kanisani baada ya kupatiwa shilingi tano.

Image: TWITTER// DCI

Jamaa wawili walikamatwa kwa kushirikiana kuteka nyara mvulana wa miaka 6  katika mtaa wa Pipeline siku ya Jumamosi .

Ezekiel Nyamawi Nyakundi na James Bundi Mabeya walikamatwa siku ya Jumatatu katika eneo la Mashimoni, mtaa wa Mathare ambako walikuwa wameweka mtoto yule.

Kulingana na DCI, wawili hao walimteka nyara Collins Orina wakati alikuwa anacheza na rafiki yake nje ya kanisa  la Kware SDA. 

Inaripotiwa kuwa mmoja wa watekaji nyara hao ambaye alikuwa amejifanya mshirika wa kanisa ile alienda kwa wavulana hao wawili walipokuwa wanacheza na kuwaahidi kuwa angewanunulia 'Chipo' (viazi) iwapo wangemfuata.

Orina alikubali kumfuata jamaa yule na wakatoweka  ila rafiki yake akarejea kanisani baada ya kupatiwa shilingi tano.

Baada ya kugundua kuwa mwanawe alikuwa amepotea, Bi Regina Bayani alienda kupiga ripoti katika kituo cha polisi cha Embakasi huku akiwa amejawa na wasiwasi. Hapo juhudi za kusaka mtoto yule zikang'oa nanga.

Kulingana na DCI, washukiwa walikuwa wameacha mtoto yule pekee yake ndani ya chumba chao katika mtaa wa Mathare ila akaamua kutoka nje kucheza na watoto wengine baada ya kuchoka kukaa kwa nyumba.

Wapelelezi walimpata Orina akicheza na wakavizia washukiwa katika chumba chao wakasubiri kuwakamata pindi watakapokuwa wanarudi.

Baada ya Nyamawi na Bundi kukamatwa, uchunguzi wa awali ulibaini kuwa wao ndio washukiwa wakuu wa matukio mengi ya utekaji nyara ambayo yamekuwa yakifanyika katika eneo la Pipeline hivi karibuni.

Bi Regina alijawa na bashasha kumuona tena mtoto wake ambaye kupotea kwake kulikuwa kumempatia wasiwasi mkubwa.