Mzozo wa kazi kati ya walevi wawili waacha mmoja akiwa mauti Bomet

Muhtasari

•Peter Ekai (30) na Elphas Kipkoech (26) walikuwa wanakata maji kwenye baa moja iliyo katika eneo Longisa, Bomet wakati mzozo huo ulitokea.

•Ekai anaripotiwa kuambia Kipkoech kwamba alikuwa amegundua kuwa alitaka apigwe kalamu katika shirika la usalama la ChapChap ili achukue nafasi yake baadae

•Vita ya maneno iligeuka  kuwa ya silaha zenye makali huku wote wawili wakidungana kwenye viungo mbalimbali za mwili.

Crime scene
Crime scene

Jamaa mmoja alipoteza maisha yake baada ya kudungwa kifuani na mwenzake kufuatia mzozo wa kazi  uliotokea jioni ya Jumapili.

Peter Ekai (30) na Elphas Kipkoech (26) walikuwa wanakata maji kwenye baa moja iliyo katika eneo Longisa, Bomet wakati mzozo huo ulitokea.

Kulingana na DCI, wawili hao walianza kuzozana baada ya Ekai kudai kwamba Kipkoech alikuwa anapanga njama ya kumpokonya kazi yake ya ulinzi katika shirika moja la usalama lililo maeneo ya Kamagut.

Ekai anaripotiwa kuambia Kipkoech kwamba alikuwa amegundua kuwa alitaka apigwe kalamu katika shirika la usalama la ChapChap ili achukue nafasi yake baadae.

Kipkoech alikanusha madai yale na kufuatia hayo mzozo mkubwa ukaanza kati ya wawili hao ambao tayari walikuwa walevi.

Vita ya maneno iligeuka  kuwa ya silaha zenye makali huku wote wawili wakidungana kwenye viungo mbalimbali za mwili.

Ekai aliumia vibaya baada ya kudungwa kwenye kifua na kukimbizwa katika hospitali ya Moi Teaching and Referral ambako aliangamia kutokana na majeraha mabaya.

Kipkoech ambaye pia aliugua majeraha alihudumiwa na kupewa ruhusa kuenda nyumbani ila akakamatwa na polisi na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Eldoret.

Mshukiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani kushtakiwa kwa mauaji.