Majonzi ya mama! Mwanamke atafuta haki baada ya ndovu aliyekuwa amepotea njia kuua bintiye Kilifi

Muhtasari

•Makawi alisema kwamba bintiye alishambuliwa wakati alikuwa anakimbia kumfahahamisha kuhusu tembo ambao walikuwa wanarandaranda pale kijijini.

•Makawi alijawa na majonzi akieleza jinsi bintiye alikufa kifo cha uchungu na kuacha mtoto wa miaka miwili.

•Inadaiwa kwamba matukio ya wanyama pori kuvamia wakazi wa eneo hilo yamekithiri na serikali imeombwa kushughulikia suala hilo.

Marehemu Margaret Chivatsi
Marehemu Margaret Chivatsi
Image: ELIAS YAA

Mama mmoja kutoka kaunti ya Kilifi anatafuta haki na kudai fidia  kutoka kwa serikali baada ya bintiye kushambuliwa na  tembo ambaye alikuwa amepotea njia.

Mwikali Makawi ambaye amefadhaika baada ya kumpoteza bintiye Margaret Chivatsi (20) alisema kwamba tukio hilo lilitokea wakati alikuwa analisha mbuzi wake kichakani.

Makawi alisema kwamba bintiye alishambuliwa wakati alikuwa anakimbia kumfahahamisha kuhusu tembo ambao walikuwa wanarandaranda pale kijijini.

"Ndovu alikimbia akielekea mahali alikuwa. Akamdunga na pembe kutoka mgongoni ikatokea tumboni" Makawi alisema.

Makawi alijawa na majonzi akieleza jinsi bintiye alikufa kifo cha uchungu na kuacha mtoto wa miaka miwili.

"Ndovu huyo alimrusha umbali wa mita kumi kutoka mahali alivamiwa. Matumbo yake yote yalimwagika nje. Alikufa dakika tano baadae alipokuwa anahudumiwa na daktari aliyefika katika eneo la tukio. Hakuna fidia inaweza tosha lakini serikali inafaa itende jambo"Makawi alisema.

Mwendesha boda boda mmoja anayefahamika kama Kalume Kazungu alisema kwamba aliona ndovu 9 mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi karibu na shule ya upili ya Ndatani. Wanafunzi walipiga makelele walipoona ndovu wale.

Inadaiwa kwamba matukio ya wanyama pori kuvamia wakazi wa eneo hilo yamekithiri na serikali imeombwa kushughulikia suala hilo.

{Utafsiri: Samuel Maina}