Mazishi ya marehemu Orie Rogo Manduli yaahirishwa baada ya bintiye mkubwa kulazwa hospitalini

Muhtasari

•Mwanasiasa huyo wa zamani sasa atazikwa mnamo Jumamosi, Oktoba 9 nyumbani kwake katika mji wa Kitale.

•Kulingana  na ujumbe ambao ulitolewa na familia siku ya Jumapili, uamuzi wa kuahirisha hafla hiyo uliafikiwa ili kupatia Bi Elizabeth nafasi ya kupata afueni.

Orie Rogo Manduli
Image: Maktaba

Mazishi ya marehemu Orie Rogo Manduli ambayo ilikuwa inatarajiwa kufanyika tarehe 2 mwezi Oktoba haitaendelea kama ilivyokuwa imepangwa.

Mwanasiasa huyo wa zamani sasa atazikwa mnamo Jumamosi, Oktoba 9 nyumbani kwake katika mji wa Kitale. 

Hii ni baada ya binti mkubwa wa marehemu, Elizabeth Rogo kulazwa katika hospitali ya Nairobi baada ya kuugua maradhi ambayo hayajathibitishwa.

Kulingana  na ujumbe ambao ulitolewa na familia siku ya Jumapili, uamuzi wa kuahirisha hafla hiyo uliafikiwa ili kupatia Bi Elizabeth nafasi ya kupata afueni.

"Familia imeangazia hali ilivyo na kuamua kuahirisha mazishi yajayo na wiki moja ili kupatia Elizabeth nafasi ya kupata afueni na aweze kuzika mama yake" Ujumbe uliokuwa umetiwa saini na msemaji wa familia Gor Semelango ulisoma.

Kufuatia hayo kutakuwa na ibada za misa ambazo zitafanyika katika kanisa la All Saints Cathedral (Nairobi) na St Stephens Cathedral (Kitale)  mnamo tarehe 5 na 6 Oktoba mtawalia.

Familia imetangaza kwamba hafla ya kuchanga fedha za kuandaa mazishi ya Manduli itafanyika siku ya Jumamosi.