Ondoeni ODM kwenye uchaguzi wa 2022 kutokana na machafuko ya Kisumu-UDA

Muhtasari
  • Seneta huyo wa zamani wa Machakos pia alikashifu Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano kwa kusalia kimya kuhusu suala hilo

Mwenyekiti wa UDA Johnson Muthama ameitaka IEBC kutoa chama cha ODM kutoka kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao.

Haya yanajiri kufuatia mtafaruku uliomlazimu Naibu Rais William Ruto kukatiza hotuba yake huko Kondele, Kisumu, baada ya vijana wenye ghasia kuwarushia mawe wasaidizi wake.

Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, Muthama alisema tukio hilo ni dhibitisho kwamba serikali iliachana na jukumu lake la kuwalinda raia.

"Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inafaa kuchukua hatua na kupa adabu chama cha ODM kwa hata kuwanyima haki ya kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao," MUthama alisema.

Seneta huyo wa zamani wa Machakos pia alikashifu Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano kwa kusalia kimya kuhusu suala hilo na kutotenda kwa njia ambayo ingewapa imani.

Aliongeza kuwa tukio hilo linafaa kuwa mwamko kwa Wakenya na wale waliopewa jukumu la kuhakikisha uchaguzi wa amani na mpito unafanyika.

"Ni siku ambayo iliwakumbusha Wakenya wanaopenda amani kwamba siku za giza za "kanda za Kanu" wakati vyama vya upinzani vilizuiwa kufanya kampeni katika baadhi ya maeneo ya nchi hazijawahi kutoweka."

Muthama alitupilia mbali taarifa ya awali ya polisi akisema kuwa DP alikuwa ameonywa kuhusu uwezekano wa vurugu ikiwa angeendelea na ziara yake katika eneo hilo.

"Swali ambalo polisi wanapaswa kujibu ni lini walijua machafuko hayo na walifanya nini ili kuhakikisha kupigwa mawe hakufanyiki na kukomeshwa," aliuliza Muthama.

Siku ya Jumatano, msemaji wa Polisi Bruno Shioso alisema kulikuwa na mvutano katika eneo la Kondele, kutokana na madai ya usambazaji wa fedha za vifaa vya kampeni miongoni mwa makundi ya wenyeji.