Maandamano dhidi ya HELB yamesitishwa! - Babu Owino

Muhtasari

• Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amesema kwamba maandamano ambayo yaliratibiwa kuanza Alhamisi Februari 10 yamesitishwa.

• Taarifa hizi kulingana na mbunge huyo mwenye utata ni kutokana na bodi ya HELB kuachilia mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kama alivyoiagiza mwishoni mwa wiki jana.

Babu Owino
Image: Facebook

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amesema kwamba maandamano ambayo yaliratibiwa kuanza Alhamisi Februari 10 yamesitishwa.

Taarifa hizi kulingana na mbunge huyo mwenye utata ni kutokana na bodi ya HELB kuachilia mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kama alivyoiagiza mwishoni mwa wiki jana.

“Ningependa kuchukua fursa hii kupongeza bodi ya HELB kwa kuachia mikopo kwa wanafunzi katika muda unaostahili.

Pili ningependa kuchukua nafasi hii kusitisha maandamano ambayo tulikuwa tumeratibu kuanza kesho Alhamisi 10, kwa sababu HELB angalau wametia jitihada.

Mwisho ninataka kutoa onyo kwa bodi ya HELB na wizara ya fedha kwamba wasijaribu kucheza na maisha ya wanafunzi wa vyuo vikuu na wakati mwingine wanajukumika kuachia hiyo mikopo kwa muda mwafaka ili wanafunzi waweze kuendeleza masomo yao,” alisema Babu katika video ambayo aliipakia mitandaoni.

Mbunge huyo pia amewahakikishia wanafunzi wale ambao hawajafanikiwa kupata mikopo hiyo kwamba amezungumza na mkurugenzi mkuu wa bodi ya HELB na kumhakikishia kwamba pesa hizo zitaachiliwa na kuwafikia wote wanaonufaika na mikopo hiyo.

Mwishoni mwa wiki jana, Owino alitoa makataa ya siku saba kwa bodi ya HELB na wizara ya fedha kutoa mikopo hiyo iliyocheleweshwa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu la sivyo, angeongoza maandamano ya kitaifa kushinikiza bodi hiyo kutii agizo lao.