HELB: Babu Owino kuongoza maandamano kwa kuchelewesha pesa

Muhtasari

• Mbunge wa Embakasi Mashariki ameahidi kuongoza wanafunzi wa vyuo vikuu kote nchini katika maandamano iwapo wizara ya fedha kwa ushirikiano na bodi ya mkopo wa elimu ya juu HELB hawatakuwa wamewapa wanafunzi mkopo huo

• Mbunge huyo ambaye alikuwa kiongozi wa wanafunzi wa chuo cha Nairobi kwa muda mrefu amesema kwamba wizara ya fedha na bodi ya mikopo hiyo imefanya maisha ya wanafunzi wa vyuo vikuu kuwa ngumu kwa kuchelewesha mikopo ya HELB

Babu Owino
Image: Facebook

Mbunge wa Embakasi Mashariki ameahidi kuongoza wanafunzi wa vyuo vikuu kote nchini katika maandamano iwapo wizara ya fedha kwa ushirikiano na bodi ya mkopo wa elimu ya juu HELB hawatakuwa wamewapa wanafunzi mkopo huo ambao umecheleweshwa kwa muda sasa.

Mbunge huyo ambaye alikuwa kiongozi wa wanafunzi wa chuo cha Nairobi kwa muda mrefu amesema kwamba wizara ya fedha na bodi ya mikopo hiyo imefanya maisha ya wanafunzi wa vyuo vikuu kuwa ngumu kwa sababu ya kuchelewesha mkopo huo ambao wengi wanautegemea kuendesha maisha yao chuoni.

Katika mkanda wa video ambao mbunge huyo amepakia katika ukurasa wake wa Facebook, Owino ametoa makataa ya siku saba kwa wizara ya fedha na bodi ya mikopo ya elimu ya juu kutoa mikopo hiyo kwa wanafunzi la sivyo ataongoza wanafunzi hao katika maandamano kote nchini ili kuishrutisha serikali kutoa mikopo hiyo.

“Tumetoa makataa ya siku saba ili mikopo hiyo itolewe kabla ya Alhamisi 10, na iwapo hawatatii amri hii, tutaandaa maandamano makubwa nchini. Barabara zote zitafungwa na tutatatiza kila shughuli kote nchini.

Kila chuo katika kila kaunti lazima wajiunga katika maandamano hayo ili kutuma ujumbe kwa serikali kwa kukataa kuwapatia wanafunzi pesa ilhali wanatakiwa kusoma.

Maandamano yetu yatakuwa ya amani na hivyo hatutegemei polisi kututupia vitoza machozi,” anasikika akisema mbunge huyo mwenye utata.

Babu Owino ameataka wanafunzi katika vyuo vyote nchini kutumia chakula kile kidogo wako nacho na kujiandaa kwa maandamano makubwa wiki kesho.

“Nawataka wanafunzi wote kuanzia leo, kuanzia sasa, jiandae, kunywa maji kwa sababu hakuna chakula. Weka kila kitu tayari kwa sababu ya siku hiyo kubwa. Tukutane Alhamisi. Ahsante sana,” Babu anasema.