Koome,Haji walaani unyanyasaji wa dereva wa kike Forest Road

Muhtasari
  • Koome,Haji walaani unyanyasaji wa dereva wa kike Forest Road
  • Wakenya wengine pia wamelaani matukio hayo wakiyataja kuwa ya kinyama
Jaji mkuu Martha Koome
Image: Twitter

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma imewataka Wakenya kuepuka kuchukua sheria mkononi.

ODPP Noordin Haji alikashifu kunyanyaswa kwa dereva wa kike kando ya barabara ya Wangari Maathai siku ya Ijumaa.

Aidha, Haji alisema kuwa uchunguzi wa polisi unaendelea na watakaobainika kuwa na hatia watafunguliwa mashtaka.

“Inasikitisha kwamba tunalazimika kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia katika wiki hiyo hiyo tunapoadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake. Wanawake na wasichana wanahitaji kulindwa na kutofanyiwa vitendo hivyo vya kinyama na vya udhalilishaji."

Wakenya wengine pia wamelaani matukio hayo wakiyataja kuwa ya kinyama.

Jaji Mkuu Martha Koome pia ameeleza kutoidhinisha hali hiyo.

Katika taarifa yake Jumanne, CJ alisema hatua za waendesha bodaboda hazifai, na kuongeza kuwa wahusika wanapaswa kukabiliwa na sheria.

"Ninatumai kuwa wahusika watakamatwa na kushughulikiwa kupitia mfumo wa haki ya jinai kwa utaratibu na kwa mujibu wa Katiba na sheria," Koome alisema.

Zaidi ya hayo, alisema wanawake, wasichana na raia wote wa Kenya lazima walindwe na akahimiza mashirika kuweka hatua za kukomesha visa vya unyanyasaji wa kingono na kijinsia.

Kisa hicho kilitokea katika barabara ya Wangari Maathai mnamo Ijumaa lakini suala hilo lilidhihirika Jumatatu baada ya video hiyo kusambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii.

Kufikia sasa zaidi ya waendesha bodaboda 200 wameiwa mbaroni kutokana na tukio hilo.