Waendesha boda boda 32 wakamatwa kwa kudhulumu dereva wa kike Forest Road

Muhtasari

•Tukio hilo la kuchukiza lilikuwa gumzo kuu mitandaoni siku ya Jumatatu baada ya video inayoonyesha yaliyojiri kusambazwa mitandaoni.

•Mwanadada huyo aliokolewa na polisi wa trafiki ambao walifikishiwa habari na madereva wengine waliokuwa wameshuhudia drama hiyo

Bodabodas
Bodabodas
Image: MAKTABA

Washukiwa 32 wamekamatwa kuhusiana na shambulio la dereva mwanamke katika barabara ya Wangari Maathai, polisi wamesema.

Kulingana na msemaji wa polisi Bruno Shioso, maafisa kutoka jijini Nairobi wanaendeleza msako wa washukiwa zaidi.

Shioso alisema kuwa washukiwa waliotiwa mbaroni watafikishwa mahakamani Jumatano.

"Nilikuwa nimetaja kuwa waendesha bodaboda 16 walikamatwa lakini kufikia sasa, idadi imeongezeka hadi takriban 32, huku takriban pikipiki 12 zikiwa zimezuiliwa," Shioso alisema akiwa kwenye mahojiano na Citizen TV. 

"Tuna viongozi vidokezo vizuri sana, unamkamata mmoja au wawili wanakupeleka kwa wengine." Alisema.

Hapo awali ilikuwa imeripotiwa kuwa washukiwa 16 wametiwa mbaroni kuhusiana na tukio hilo lililotokea Ijumaa.

Tukio hilo la kuchukiza lilikuwa gumzo kuu mitandaoni siku ya Jumatatu baada ya video inayoonyesha yaliyojiri kusambazwa mitandaoni.

Msemaji wa Polisi alithibitisha kwamba mwanamke huyo alipiga ripoti kuhusu kisa hicho hapo  awali lakini kwa kuwa alikuwa na kiwewe ilibidi aende nyumbani na kuripoti tena Jumatatu.

Kwenye taarifa ambayo aliandikisha katika kituo cha polisi cha Parklands , mwanamke huyo alieleza kuwa mwendesha bodaboda mmoja alizuia gari lake ghafla na akagonga pikipiki yake.

Mwendesha bodaboda huyo alianguka chini na kuvunjika mguu.

Alisimama mita chache kutoka kwa eneo la tukio, lakini akazingirwa na kundi la waendesha bodaboda ambao baadhi yao walijaribu kumwibia.Alishtuka na kuendelea na safari yake. 

Waendesha bodaboda hao walimfuata kwa kilomita chache na kulizuia gari lake. Kisha wakafungua mlango wa gari lake kwa nguvu na akaanza kupiga kelele akiomba msaada.

Muda huo wote mmoja wa waendesha bodaboda alikuwa anarekodi tukio hilo.

Mwanadada huyo aliokolewa na polisi wa trafiki ambao walifikishiwa habari na madereva wengine waliokuwa wameshuhudia drama hiyo. Alipoteza pesa na vitu vingine vya thamani kwenye tukio hilo.