Radi ya mauti: Watu 2 wa familia moja wamefariki baada ya kupigwa na radi Webuye

Muhtasari
  • Watu 2 wa familia moja wamefariki baada ya kupigwa na radi Webuye
KWA HISANI
KWA HISANI

Wakaazi wa kijiji cha Malaha kaunti ya Bungoma wanataabika baada ya familia moja kuwapoteza jamaa zao wawili kwenye mkasa wa radi Jumapili jioni.

Wawili hao Francisca Wabomba, 21, na Valary Naliaka, 13, walipigwa na radi walipokuwa wakielekea nyumbani kutoka kwenye kinu cha posho.

Akithibitisha kisa hicho, chifu Msaidizi wa eneo hilo Bramwel Kachelo alisikitika kufariki kwa wawili hao na kuwataka wazazi kutowaruhusu watoto wao kutoka nje wakati mvua inaponyesha.

Kachelo aliongeza kuwa tukio hilo lilitokea saa kumi na mbili usiku.

"Katika msimu huu, tuna mvua nyingi zinazoambatana na radi. Ninawaomba wazazi kufuatilia hali ilivyo kabla ya kuwaruhusu watoto wao kutembea nje mvua inanyesha," alisema. sema. "Ni siku ya huzuni katika eneo hili. Waliofariki ni marafiki zangu. Inatia uchungu kupoteza watoto katika umri mdogo kama huu."

Msimamizi huyo alizitaka mamlaka husika kuweka vifaa vya kuzuia radi katika eneo hilo ili kuepusha majanga hayo siku zijazo.

"Kwa uaminifu eneo hili hukumbwa na radi wakati wa mvua. Natoa wito kwa mamlaka husika kutusaidia kupata vizuizi vya umeme katika eneo hilo ili kupunguza matukio kama haya," alisema. .

Miili ya marehemu ilichukuliwa na maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Webuye na kupelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya kaunti ya Webuye kwa ajili ya kuhifadhiwa huku familia ikianza mipango ya maziko.