Miguna kuhudhuria sherehe za Mashujaa na baadaye kukutana na rais Ruto ikuluni

Jenerali huyo alitua katika uwanja wa ndege wa JKIA alfajiri ya Oktoba 20.

Muhtasari

• Aliweka wazi kwamba amepata mialio rasmi ya kuhudhuria sherehe za mashujaa na baadae atakutana na rais Ruto katika ikulu ya Nairobi.

Jenerali Miguna hatimaye ametua nchini
Jenerali Miguna hatimaye ametua nchini
Image: Andrew Kasuku

Wakili aliyekuwa uhamishoni kwa muda wa miaka 4 na ushee Dkt. Miguna Miguna hatimaye aliwasili nchini alfajiri ya Oktoba 20.

Miguna ambaye alijitangaza kama jenerali, alifurushwa nchini mnamo 2018 na licha ya majaribio kadhaa ya kujaribu kurudi nchini, hakuweza kufua dafu kwani aliwekewa vizuizi na vizingiti ambavyo havingeruhusu shirika lolote la ndege kumpa usafiri kutua nchini.

Masaibu yake yalianza Januari 2018 alipomuapisha kinara wa muungano wa NASA kipindi hicho, Raila Odinga kama rais wa wananchi na baada ya wiki chache kinara huyo akamsaliti kwa kusalimiana na rais kipindi hicho Uhuru Kenyatta katika kile kilichoashiria kuzikwa kwa tofuati kati ya viongozi hao wawili na kuahidi kufanya kazi pamoja.

Ni suala ambalo Miguna alikuwa analipinga kwa kile ambacho alisema Raila aliwasaliti watu waliosimama nyuma yake kutaka haki kutokana na kile walikuwa wanadai ni wizi wa kura za mwaka 2017 ambao ulimpokonya Raila ushindi.

Tofauti hizo zilisababisha ufa mkubwa baina ya Raila na Miguna kupelekea yeye kufurushwa nchini na hata kwa wakati mmoja alisikika akidai kwamba pasipoti yake ya usafiri ilichanwa na hivyo kumfungia kabisa dhidi ya kusafiri kurudi nchini, huku ikidaiwa kwamba ana urai wa mataifa mawili, Kenya na Kanada.

Maagizo ya mahakama ya kuagiza aruhusiwe kuingia nchini yalipuuzwa na utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Jenerali huyo wa kujitangaza mwenyewe aliwasili nchini na hata kutangaza mipango yake ya siku ambapo alionesha dhibitisho kwamba amealikwa kuhudhuria sherehe za Mashujaa zitakazofanyika leo hii na kisha baadae kukutana na rais Ruto katika ikulu ya Nairobi.

"Kuanzia JKIA hadi #MashujaaDay. Kisha kuelekea @StateHouseKenya. Wazalendo wako na uhuru kujitokeza JKIA. Uhuru uko hapa! Hongera," Miguna aliandika kwenye dhibitisho la mialiko hiyo Twitter.