Nikitua Kenya tu Octoba 20, nitacheza densi ya Vaida - Miguna Miguna

Alidhibitisha kwamba safari yake badi ingalipo na anatarajiwa kuwasili katika angatua ya JKIA Alhamisi alfajiri.

Muhtasari

• “WAZALENDO: Nitawasili kwa Ndege ya KQ saa kumi na mbili asubuhi. Terminal 1. Cheers.” Miguna Miguna aliandika kwa furaha.

Miguna Miguna
Miguna Miguna
Image: MAKTABA

Alhamisi wiki hii itakuwa ni siku yenye mishe nyingi nchini Kenya. Kando na kuwa itakuwa siku ya kusherehekea mashujaa waliopigania uhuru wa taifa la Kenya kutoka kwa wabepari, pia itakuwa siku ya kihistoria kwa wakili Miguna Miguna ambaye anatarajiwa kutua nchini baada ya kukaa uhamishoni nchini Kanada kwa zaidi ya miaka 4.

Wakili huyo ambaye ni mzungumzaji sana kwenye mtandao wa Twitter amekuwa akipakia mfululizo wa tweets akidokeza kuhusu maendeleo ya ujio wake mnamo Agosti 20.

Asubuhi ya Jumanne, wakili Miguna aliweka wazi kwamba safari yake bado inaglipo jinsi ilivyoratibiwa awali na kuwaambia watumizi wa mtandao huo kuwa atawasili katika angatua ya JKIA Alhamisi saa kumi na mbili asubuhi.

“WAZALENDO: Nitawasili kwa Ndege ya KQ saa kumi na mbili asubuhi. Terminal 1. Cheers.” Miguna Miguna aliandika kwa furaha.

Alidokeza kwamba pindi atakapowasili, hatocheza kwa ngoma nyingine bali ataikumbatia densi ya isikuti kwa ngoma ya Vaida ambayo inazidi kuteka mawimbi nchini kwa zaidi ya mwezi mzima.

“Rafiki zangu wa Mulembe wananiambia itakuwa Wimbo na Ngoma ya VAIDA mnamo Oktoba 20. HONGERA!” Miguna alidokeza huku akisema kwamba hatoweza kucheza densi ya Reggae kwa sababu ilizimwa, akionekana kuchimba mkwara kwa mswada wa BBI uliotupiliwa mbali mapema mwaka huu na mahakama ya upeo.

Alihakikishia wafuasi wake kuwa vizuizi vilivyokuwa vimewekwa dhidi yake na serikali ya awali vimeondolewa na rais William Ruto na uongozi wake.