Wakenya wa ughaibuni walalamikia benki ya Equity kuhitilafiana na michango kwa ajili ya Miguna

Wakenya hao waliteta vikali kwamba usimamizi wa benki hiyo unafanya kuwa vigumu kwa watu kufanya miamala inayolenga kufanikisha safari ya Jenerali Miguna.

Muhtasari

• Pia walimpongeza rais Ruto kwa kusimama imara dhidi ya wale waliokuwa na mipango ya kuvuruga demokrasia ya nchi na pia kufanikisha kuondolewa kwa vizuizi dhidi ya Jenerali Miguna.

Miguna Miguna afurushwa kutoka Kenya mnamo Machi 2018
Miguna Miguna afurushwa kutoka Kenya mnamo Machi 2018
Image: MAKTABA

Kundi la Wakenya wanaoishi ughaibuni haswa katika taifa la Uingereza na Marekani Kaskazini wameonesha kutoridhishwa kwao katika kile wanakitaja kuwa hatua ya benki ya Equity kuhitilafiana na miamala ya pesa zinazochangishwa kumwezesha wakili Miguna Miguna kurejea nchini.

Katika taarifa waliyoitoa kwa umma, kundi hilo likiongozwa na mwenyekiti Sebastian Onyango walisema kuwa uongozi wa benki ya Equity nchini Kenya umekuwa ukijaribu kulemaza mchakato wa kuchangishwa kwa pesa hizo kupitia nambari ya paybill 247247. Kundi hilo liliteta vikali kwamba hatua hiyo si tu inaweka vizingiti vya kulemaza michango kutoka kwa watu wa ughaibuni lakini pia imezua ugumu kwa Wakenya wanaojaribu kufanikisha michango hiyo.

“Tunashutumu kwa maneno makali iwezekanavyo namna ya kiholela ambayo mameneja katika Benki ya Equity wanaendelea kutumia nafasi zao za upendeleo kwa kuingilia kati shughuli halali ya kuchangisha pesa kutoka kwa marafiki wa Jenerali Miguna Miguna kwa kusababisha kufeli kwa mfumo na hitilafu ambazo zinatatiza majaribio ya kuingiza pesa kwenye akaunti,” sehemu ya taarifa hiyo iliyoonwa na Radio Jambo ilisoma.

Kundi hilo lilitoa makataa kwa usimamizi wa benki ya Equity na kuitaka kuondoa vikwazo vyote ambavyo vinalemaza shughuli ya kuingiza pesa zinazonuiwa kufanikisha safari ya Miguna kuja nchini mnamo Octoba 20 kama alivyoweka wazi kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Kando na malalamishi hayo, pia Wakenya hao walioko ughaibuni waliutambua mchango wa rais William Ruto kuhakikisha vikwazo vilivyowekwa kuzuia Miguna kurudi nchini vyote vimeondolewa kikamilifu.

Walisema wanamuunga mkono rais juu ya hili kwa asilimia mia katika kile walisema kwamba alisimama imara kupinga matakwa ya wale waliokuwa na malengo ya kuanzisha historia ya hatari ambayo ingewatenga wanasiasa walioonekana kuwa na mawazo pamoja na itikadi zilizokinzana na zao.

“Utawala wa sheria umezingatiwa, Haki haijatendeka tu, bali imeonekana kutendeka juu ya jambo hili. Tunataka kumtia moyo rais aendelee kushughulikia mambo mengine ya kitaifa yanayohusu utawala wa sharia,” taarifa hiyo ilisema.

Baadhi ya masuala ambayo walipendekeza rais Ruto kuzamia zaidi ni unyakuaji haramu wa bandari za Mombasa, Lamu na Kisumu pamoja pia na wale waliotumia ushawishi wao katika serikali iliyopita na kujilimbikizia mali ya umma kwa matumizi ya kibinafsi na faida.