"Tafadhali saidia serikali kumaliza baa la njaa" DP Gachagua aomba sekta binafsi

Gachagua aliwapongeza kwa kuchangisha milioni 114 katika wakfu wa Pamoja Tuungane na kuwataka wasichoke kuendelea kusaida serikali.

Muhtasari

• "Mabibi na mabwana, hali si hali tena, hali ni tete na huo ndio ukweli" Gachagua aliwaambia wafanyibiashara wa sekta binafsi katika mkutano.

Naibu Rais William Ruto
Image: TWITTER// RIGATHI GACHAGUA

Huku zaidi ya kaunti 20 humu nchini zikiwa zimeathirika na ukame pamoja na baa la njaa, Jumatatu naibu rais Rigathi Gachagua alikutana na wafanyibiashara kutoka sekta za kibinafsi ambapo aliwarai kuingilia kati ili kuisaidia serikali katika kulikabili tatizo hilo ambalo limefananishwa na janga la kitaifa.

DP Gachagua aliwapongeza sekta hiyo ya kibinafsi kwa kuchangisha zaidi ya milioni 100 kwa ajili ya kuwakwamua waathiriwa wa ukame kote nchini.

“Mmechangisha zaidi ya milioni 114 chini ya wakfu wa Pamoja Tuungane kwa ajili ya ndugu na dada zetu humu nchini wanaokumbwa na baa la njaa katika kaunti za jagwani na kwingine pia. Hii ni hatua ya kupongezwa, na kwa niaba ya serikali nasema ahsante sana” Gachagua alisema.

Rigathi aliongezea kuwa amepewa jukumu na rais Ruto ili kufanya mazungumzo na serikali za kaunti pamoja na sekta za kibinafsi za kibiashara ili kusambaza chakula katika maeneo ambayo yameathirika pakubwa, huku akiwataka wahudumu katika sekta hiyo ya kibinafsi kutochoka kuisaidia serikali kutoa msaada wa chakula.

“Mabibi na mabwana, hali si hali tena, hali ni tete na huo ndio ukweli. Kila mahali tunatuma watu kusambaza chakula, harufu ya mizoga inahanikiza, watoto wanagoma kuenda shule na Wakenya wanazidi kutamauka. Natoa wito kwenu tafadhali, ingia zaidi kwenye mifuko yenu na muone chenye mnaeza fanya ili kunusuru hali hii, ili tuwe na juhudi za pamoja kuhakikisha kuwa hakuna Mkenya hata mmoja anayekufa kwa njaa. Ninahitaji KSh bilioni 2 kwa dharura kutoka kwenu” DP Gachagua aliwaambia wafanyibiashara wa sekta ya kibinafsi.