Mwenye jumba lililoporomoka Kasarani ashtakiwe kwa mauaji - Gavana Sakaja

Wale mnaoendeleza mijengo haiijapitishwa, nataka kuwapa notisi kuwa angusha majumba hayo wenyewe kabla hatujawafikia - Sakaja.

Muhtasari

• Sisi kama kaunti tutachukua hatua na mwenye mjengo lazima ashikakiwe mahakamani - Sakaja.

Sakaja azungumzia kuporomoka kwa ghorofa Kasarani
Sakaja azungumzia kuporomoka kwa ghorofa Kasarani
Image: Facebook

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ametembelea eneo la Kasarani ambapo jumba la ghorofa 7 liliporomoka alasiri ya Jumanne na kusema mwekezaji aliyekuwa analijenga jumba hilo anastahili kushtakiwa kwa mauaji.

Alisema kuwa mwenye jumba hilo alikuwa amepewa notisi ya kutoendelea na ujenzi ila akapuuza katika kile ambacho alikitaja kuwa ni ufisadi usiomithirika na ukaidi wa sheria.

“Jana NCA walikuwa hapa na walikuwa hapa na walifunga mjengo kutoendelea, lakini mwanakandarasi anajua kwamab katika kesi kama hizi mtu unaendelea tu na ujenzi na kuwalipa watu wachache hapa na pale. Sisi kama kaunti tutachukua hatua na mwenye mjengo lazima ashikakiwe mahakamani, tutashirikiana na polisi na anafaa kushtakiwa kwa mauaji,” Gavana Sakaja alinguruma.

Pia alitoa onyo kwa wajenzi wote ambao wanajua wanaendeleza mijengo kama hiyo ambayo haijakidhi mahitaji yote kutoka kwa idara za ujenzi kuchukua tahadhari na kukoma mara moja kwa sababu hiyo ni kama kuchimba kaburi la kuwazika mamia ya watu ambao baadae watakuja kuishi na kufanya biashara zao katika mijengo kama hiyo jijini Nairobi.

“Nataka kuwaambia wote wale ambao wanaendeleza mijengo ambayo haijapitishwa, nataka kuwapa notisi kuwa angusha majumba hayo wenyewe kabla hatujawafikia. Kwa sababu mnahatarisha maisha ya watu,” Gavana Sakaja alisema.

Katika kuporomoka kwa jumba hilo mtaani Kasarani, shughuli za uokoaji zilianza mara moja ambapo mpaka mchana wa Jumatano, tayari miili ya watu 3 ilikuwa imetolewa kwenye vifusi vya jumba hilo. Watu 6 walikuwa wameokolewa.