Familia ya mwanamitindo Chiloba yakanusha madai alikuwa mwanachama wa LGBTQ

Jackton Odhiambo alikiri kumuua mwanamitindo huyo kwa madai ya kumsaliti.

Muhtasari
  • Washukiwa watano kufikia sasa wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya Chiloba akiwemo mmoja aliyekiri kuwa mpenzi wake
Jackton Odhiambo na Edwin Chiloba
Image: INSTAGRAM

Familia ya mwanaharakati wa LGBTQ aliyeuawa Edwin Kiprotich Kiptoo almaarufu Chiloba imewataka Wakenya kukoma kueneza habari za uwongo kumhusu kwenye mitandao ya kijamii.

Katika mahojiano Jumatatu na NTV, binamu yake Gaudencia Tanui alisema Chiloba alikuwa mtu anayempenda Mungu tangu miaka yake ya ujana kinyume na picha ya mtu asiye na maadili inayochorwa kumhusu.

"Alikuwa mvulana mwenye maono. Alikuwa kiongozi wa kanisa katika Shule ya Msingi ya Sergoit alikohudhuria. Katika St Francis Kimuron alipewa jina la utani pasta kwa sababu alikuwa mtoto wa kanisa," alisema.

"Haya mambo ambayo tunasikia yakienea social media, wakenya wenzangu tafadhali, muache kueneza mambo ambayo hayana ukweli na ambayo si ya ubinadamu. Tunaumia kama familia," Gaudencia alisema.

Washukiwa watano kufikia sasa wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya Chiloba akiwemo mmoja aliyekiri kuwa mpenzi wake.

Jackton Odhiambo alikiri kumuua mwanamitindo huyo kwa madai ya kumsaliti.

Aliambia polisi mjini Eldoret kwamba alimuua mwanamitindo huyo wa kiume kama kulipiza kisasi kwa kumsaliti.

Odhiambo, ambaye alikamatwa Ijumaa, alisema amekuwa akiishi na Chiloba kwa kipindi cha mwaka mmoja kama mume na mke.

Lakini Tanui alipuuzilia mbali madai kwamba Chiloba alikuwa shoga.