KWS yatetea upasuaji wa vasektomi kwa simba

KWS ilisema utaratibu huo ulikusudiwa kudhibiti kizazi cha simba huyo

Muhtasari

•Lakini KWS imeeleza kwamba paka huyo mkubwa atakuwa katika mazingira magumu porini.

Image: BBC

Shirika la Huduma ya Pori la Kenya (KWS) wikendi lilieleza ni kwa nini simba aliyenaswa alilazimika kufanyiwa upasuaji vasektomi mwanzoni mwa wiki jana.

Awali KWS ilisema utaratibu huo ulikusudiwa kudhibiti kizazi cha simba huyo, lakini Wakenya walihoji ni kwa nini hangeweza badala yake kumuachilia porini huku kukiwa na hatari ya wanyama hao kuangamia .

Lakini KWS imeeleza kwamba paka huyo mkubwa atakuwa katika mazingira magumu porini.

“Wanyama wa porini wanapofugwa , hupoteza silika yao ya asili na wakirudishwa porini, wanakuwa hatarini.Paka hao huishia kuwa wanyama wenye matatizo wanapotafuta mawindo rahisi,” ilisema taarifa.

KWS ilisema mzozo kati ya binadamu na wanyamapori unaosababisha majeraha na mauaji ya kulipiza kisasi ni miongoni mwa tishio kuu kwa uhifadhi wa simba nchini.

Kwa sasa, idadi ya simba nchini Kenya inakadiriwa kuwa 2,589, kulingana na KWS.