Githurai: Jambazi auawa akiwa katika harakati ya kumuibia mtu kwenye lango lake

Baada ya kumaliza kumuibia mwanamume huyo, jambazi huyo aliruka kwa pikipiki ya mwenzake na wakachana mbuga, lakini walikutana na polisi...

Muhtasari

• Tukio zima jinsi walimuibia mzee huyo lilishuhudiwa katika kamera za siri, CCTV za makazi hayo.

Picha za CCTV jinsi mwanamume huyo alivamiwa na jambazi.
Picha za CCTV jinsi mwanamume huyo alivamiwa na jambazi.
Image: Facebook//DCI

Makachero wa DCI usiku wa Ijumaa walimpiga risasi na kumuua jambazi sugu aliyekuwa akimuibia mkaazi mmoja wa mtaa wa Githurai katika kaunti ya Kiambu.

DCI kwa kuchagiza mno kama kawaida yao, walihadithia kisa hicho kwenye mitandao ya kijamii wakisema kwamba jambazi huyo alimvamia mwanamume mmoja aliyekuwa na gari lake akiingia katika makazi yake Githurai 44.

Mwanamume huyo alishuka kufungua mlango wa kuingia kwenye makazi kabla ya jambazi huyo kuchomoka kutoka kwa kichaka cha giza kilichoko karibu na makazi hayo kabla ya kumunyooshea mwanamume huyo bunduki akimtaka kutoa kila kitu mfukoni mwake.

Baada ya kumaliza shughuli yake ya kumuibia, katika kile kilionekana kama tukio lililokuwa limeratibiwa, mwenzake aliwahi kwa haraka na pikipiki ambapo jambazi wa kwanza aliruka na kuparamia juu na wakaondoka eneo la tukio wakimuacha mzee wa watu hoi bin taaban kwenye lango la makazi hayo.

Majambazi hao hawakujua kwamba eneo walimokuwa wakitorokea ndiko maafisa wa polisi waliokuwa walikuwa wanapiga doria.

“Na maafisa hao walifuata pikipiki hiyo mbuo, jambazi huyo mwenye silaha alishuka ghafla na kuanza kukimbia kwa miguu kuelekea kwenye njia ya miguu huku akiwafyatulia risasi maafisa hao. Bila chaguo lingine, mmoja wa washambuliaji wa uhalifu alifyatua risasi na kumnyamazisha, na kumaliza harakati hizo,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

Hata hivyo, jambazi wa kwanza alifanikiwa kutoroka na pikipiki huku mwili ya huyo mmoja ukilazwa katika hifadhi ya maiti ya City jijini Nairobi ukisubiri kutambuliwa.