Jeff Mwathi aliuawa na wala hakujiua kwa kujirusha kutoka ghorofani - DCI wabaini

Maafisa wa upelelezi wa jinai DCI walibaini kwamba hakuna uwezekano wa mtu mzima kutoshea dirisha dogo la chumba hicho alikodaiwa kujirusha.

Muhtasari

• DCI walisema wamekamilisha awamu ya kwanza ya uchunguzi wa kifo cha kijana huyo mbunifu wa mapambo na kufutilia mbali dhana kuwa alijiua mwenyewe.

• Awamu ya pili itaanza hivi karibuni ambapo wote waliokuwemo ndani ya nyumba ya Fatxo na Jeff watahojiwa.

Mwimbaji DJ Fatxo na marehemu Jeff Mwathi
Image: HISANI

Mbunifu wa mapambo Jeff Mwathi aliuawa na hakujirusha kutoka ghorofa ya kumi kama ilivyoripotiwa awali.

Haya yamebainika baada ya idara ya upelelezi wa jinai DCI kukamilisha awamu ya kwanza ya uchunguzi kuhusiana na kifo hicho tata ambacho kimevutia wengi mitandaoni wakitaka haki kutendeka.

Uchunguzi huo ulianzishwa wiki moja iliyopita upya na maafisa wa idara ya DCI, kufuatia agizo la waziri wa usalama wa ndani Profesa Kithure Kindiki kumtaka mkurugenzi wa idara hiyo Amin kutuma wapelelezi wa mauaji ya kinyumbani kufanya uchunguzi huo ambao wengi wa Wakenya walihisi ulihitilafiwa na kufanywa kwa njia isiyofaa na maafisa wa kituo cha polisi cha Kasarani awali.

Baada ya awamu ya kwanza ya uchunguzi wa DCI kukamilika, walibaini kwamba kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 aliuawa nqa hakujirusha kutoka ghorofani kama ilivyodaiwa.

Maafisa hao wa DCI pia walibaini kwamba kabla ya kuuawa, kulikuwa na mapambano makali ndani ya nyumba hiyo anakoishi msanii maarufu wa Mugithi Lawrence Njuguna maarufu DJ Fatxo.

Kulingana na ripoti hiyo iliyopeperushwa na runinga ya Citizen, wapelelezi walitupilia mbali dhana na uwezekano wa kujiua kwa kujitupa mwenyewe kutoka dirisha la chumba cha kulala kama DJ Fatxo alivyodai, kwani hakuna uwezekano hata kidogo wa mtu mzima kutoshea katika dirisha hilo.

Asubuhi hiyo ya tarehe 23 Februari wakati wa kifo cha Jeff, watu 5 walionekana ndani ya nyumba ya Fatxo iliyoko Roysambu akiwemo Mwathi na maafisa walisema wote waliokuwemo naye usiku huo watafanyiwa usaili wa kina ili kutoa upande wao wa matukio yalivyokuwa.

Kand na hao, pia maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Kasarani waliofika wa kwanza katika eneo la mkasa watatakiwa kufika katika makao makuu ya DCI kwa usaili na mahojiano ya kina.