Uhuru awadhubutu waasi kuondoka Jubilee

Hii ni baada ya mzozo kuzuka hapo awali katika afisi za Jubilee baina ya wafuasi wa Kanini Kega na Jeremiah Kioni.

Muhtasari

• Uhuru aliwashauri polisi kutekeleza majukumu mengine muhimu ya kitaifa. 

Image: Maktaba

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ametoa msimamo wake  kuhusiana na mzozo katika chama cha Jubilee.

Uhuru ambaye ndiye kinara wa chama hicho alilazimika kufika katika ofisi za Jubilee siku ya Jumatano wakati mzozo ulikuwa  ukitokota.

Alishukuru baadhi ya wanachama ambao alisema wameshikilia chama hicho na kuwataka wale ambao wanataka kuondoka kufanya hivyo kwa njia ya amani huku akisema wanachofanya ni kulinda chama chao cha Jubilee.

"Nawashukuru kwa kulinda chama chenu, sisi hatuna vita na mtu, na wale ambao hawataki waende kule wanakotaka kwa amani," Kenyatta aliwaambia baadhi ya wanachama.

Awali katibu mkuu wa chama hicho na wafuasi wake walikuwa wamezuiwa kuingia katika afisi hizo.  Kiongozi wa wachache Opiyo Wandayi na viongozi wengine wa ODM pia walinyimwa nafasi kuingia.

Baadhi ya wanachama wa chama cha Jubilee waliteta kuwa ODM haifai kuingilia masuala ya Jubilee. Hii ni baada ya Mahakama ya Vyama vya Kisiasa kukataa kufutilia mbali hatua ya NEC iliyomteua mbunge wa EALA Kanini Kega kuhudumu kama katibu mkuu wa chama hicho. 

Kenyatta pia aliwasuta maafisa wa polisi akisema wana kazi zaidi ya kufanya kuliko kusumbua watu katika vyama vyao huku akiwakashifu wanaojaribu kuwanyanganya chama.

"Polisi fuateni haki,tumewaona mara kadhaa mkienda njia ya kukosa kufuata haki,tendeni haki,mliapa ya kwamba mtalinda nchi pamoja na wananchi na katiba.Nimekuja kusimama na wanachama wetu,kusimama na haki,sina jambo jingine," alisema Kenyatta.

Kadhalika,Kenyatta alisema wao wamekodesha tu afisi za Jubilee eneo hilo wala hawana umiliki wa majengo hayo