Uhuru awasili katika makao makuu ya Jubilee baada ya makabiliano kushuhudiwa

Hii ni baada ya Mahakama ya Vyama vya Kisiasa kukataa kufutilia mbali hatua ya NEC lililomteua Kega kuchukua nafasi yake.

Muhtasari
  • Wafuasi hao walionekana wakipiga mawe katika makao makuu ya afisi ya Jubilee huko Kileleshwa.
Image: HISANI

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta amewasili katika makao makuu ya Jubilee Kileleshwa huku kukiwa na makabiliano.

Hii ni baada ya machafuko kushuhudiwa katika afisi ya makao makuu ya Jubilee baada ya wafuasi wa kaimu katibu mkuu Kanini Kega na katibu mkuu aliyesimamishwa kazi Jeremiah Kioni kuzozana.

Wafuasi hao walionekana wakipiga mawe katika makao makuu ya afisi ya Jubilee huko Kileleshwa.

Kulikuwa na msururu mkubwa wa polisi katika eneo hilo.

Walitumia vitoa machozi kuwatawanya wafuasi hao.

Baadhi ya wanachama wa chama cha Jubilee waliteta kuwa ODM haifai kuingilia masuala ya Jubilee.

Hii ni baada ya Mahakama ya Vyama vya Kisiasa kukataa kufutilia mbali hatua ya NEC lililomteua Kega kuchukua nafasi yake.

Katika hukumu yake iliyotolewa Aprili 16, mahakama hiyo ilisema notisi ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa iliyotolewa Februari 2 na NEC iliyofuata Februari 10 iliyomtaka Kega ilifanyika kwa mujibu wa Katiba ya chama.

Katika kutoa uamuzi huo, mahakama hiyo ilisema Kioni alishindwa kwanza kutafuta suluhu la mgogoro kuhusu kikao cha NEC mbele ya Kamati ya Utatuzi wa Migogoro ya Ndani ya Chama (IDRC).