Mzozo washuhudiwa katika afisi za Jubilee,Kileleshwa

Muhtasari

•Baadhi ya wanachama wa chama cha Jubilee waliteta kuwa ODM haifai kuingilia masuala ya Jubilee

Mzozo wazuka katika afisi za Jubilee baina ya Kioni na Kega.
Mzozo wazuka katika afisi za Jubilee baina ya Kioni na Kega.
Image: HISANI

Mzozo ulishuhudiwa Jumatano kati ya kaimu katibu mkuu wa Jubilee Kanini Kega na wafuasi wa katibu mkuu Jeremiah Kioni.

Kiongozi wa wachache Opiyo Wandayi na viongozi wengine wa ODM pia walinyimwa kuingia afisini. Kulikuwa na msururu mkubwa wa polisi katika eneo hilo. Walitumia vitoa machozi kuwatawanya wafuasi wa Kioni na Kega.

Wafuasi wa Kioni walikuwa wakijaribu kulazimisha kuingia katika makao makuu ya Jubilee lakini wakazuiwa kuingia. Kiongozi wa wachache Opiyo Wandayi na viongozi wengine wa ODM pia walinyimwa kuingia afisini.

Baadhi ya wanachama wa chama cha Jubilee waliteta kuwa ODM haifai kuingilia masuala ya Jubilee. Hii ni baada ya Mahakama ya Vyama vya Kisiasa kukataa kufutilia mbali hatua ya NEC lililomteua Kega kuchukua nafasi yake.

Katika hukumu yake iliyotolewa Aprili 16, mahakama hiyo ilisema notisi ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa iliyotolewa Februari 2 na NEC iliyofuata Februari 10 iliyomtaka Kega ilifanyika kwa mujibu wa Katiba ya chama.

Katika kutoa uamuzi huo, mahakama hiyo ilisema Kioni alishindwa kwanza kutafuta suluhu la mgogoro kuhusu kikao cha NEC mbele ya Kamati ya Utatuzi wa Migogoro ya Ndani ya Chama (IDRC).

"Katika hatua hiyo, tunakataa mwaliko wa kutoa tamko la ubatili wa notisi iliyotolewa na wahusika wa tarehe 2 Februari 2023, ajenda, maazimio na barua ya Februari 10, 2023," mahakama hiyo iliamua.

Hata hivyo, mahakama hiyo ilisema kuwa barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya Februari 13 iliyotambua kuteuliwa kwa Kega kama katibu mkuu mpya ilikiuka sheria. Ilisema Msajili alishindwa kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa inayotaka jambo ambalo liko mbele ya utaratibu wa utatuzi wa migogoro ya ndani ya chama lisikilizwe na kuamuliwa kwanza kabla hajatoa maagizo yoyote.