Watu watatu wamefariki baada ya tuk-tuk kugongana na lori Kilifi

Wawili kati ya waliofariki ni watu wa ukoo.

Muhtasari

• Watu wengine watatu katika tuk-tuk wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Kilifi. Wawili wako katika hali mbaya.

• Fredrick Kadzo, mkazi, alipoteza wapendwa wawili katika ajali hiyo.

Image: STAR

Watu watatu walifariki Jumatatu usiku baada ya tuk-tuk waliyokuwa wakisafiria kugongana na lori eneo la Kwakazuri kando ya barabara kuu ya Kilifi-Malindi.

Watu wengine watatu katika tuk-tuk wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Kilifi. Wawili wako katika hali mbaya.

Kamanda wa polisi wa gatuzi Ndogo ya Kilifi Kaskazini Kenneth Maina alisema watu wawili akiwemo dereva wa tuk-tuk walifariki papo hapo huku mtu wa tatu akiaga dunia alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kilifi.

Wawili kati ya waliofariki ni watu wa ukoo.

“Tuk-tuk ilikuwa imejaa kupita kiasi na ilikuwa ikielekea Tezo kutoka Kilifi. Ilikuwa na watu sita akiwemo dereva. Dereva wa tuk-tuk alikuwa akipita trela na kugongana uso kwa uso na lori hilo,” alisema.

Maina Alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa nne usiku.

Fredrick Kadzo, mkazi, alipoteza wapendwa wawili katika ajali hiyo.

Kulingana na Kadzo, jamaa zake Edgar Kadzo na Kilian Chiro wote ni madereva wa tuk-tuk.

“Edgar ni kaka yangu na Chiro ni mpwa wangu. Wote ni madereva wa tuk-tuk na walikuwa wakielekea nyumbani ajali ilipotokea," alisema.

"Walikuwa wamechukua abiria huko Kilifi na walitakiwa kuwafikisha Tezo na kisha kuelekea nyumbani. Nilizungumza nao jioni na saa 10:30 jioni nikapokea taarifa za kufariki kwao. Ni uchungu mkubwa kupoteza wapendwa wangu kwa wakati mmoja."

Miili hiyo ilihamishwa hadi katika makao ya maiti ya hospitali ya kaunti ya Kilifi ikisubiri uchunguzi wa maiti.