Tunajua kuendesha uchumi-Raila amwambia Ruto

Azimio chini ya uongozi wa Raila alitaja hatua hizo kuwa "daraja kuu katika kumfanya kila Mkenya awe mnyonge."

Muhtasari
  • Kiongozi huyo wa ODM alimweleza Rais William Ruto kwamba anapinga Mswada wa Fedha kwa sababu amewahi kuwa serikalini na anajua jinsi uchumi unavyoendeshwa.
KINARA WA MUUNGANO WA AZIMIO RAILA ODINGA
Image: TWITTER

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga ameendeleza matamshi yake ya kupinga Mswada wa Fedha na kuwataka Wakenya kupinga mapendekezo ya hatua za ushuru kwa gharama yoyote.

Akizungumza Jumatano wakati wa Mpango wa Kuwawezesha Vijana na Wanawake wa Nairobi, Raila alisema amewaagiza wabunge washirika wa Azimio kutupilia mbali Mswada huo ukifika katika ukumbi wa Bunge kwa ajili ya kupiga kura.

“Jana nilikuwa hapa na wabunge wetu nikawaambia sitaki kuona hata mbunge mmoja anaunga mkono, nataka wabunge wetu wasimame wahesabiwe,” alisema.

"Tutahesabu watakaopinga na watakaounga mkono ili wapiga kura waliowachagua wajue wasaliti ni akina nani."

Kiongozi huyo wa ODM alimweleza Rais William Ruto kwamba anapinga Mswada wa Fedha kwa sababu amewahi kuwa serikalini na anajua jinsi uchumi unavyoendeshwa.

Alisema katika kipindi chake cha Uwaziri Mkuu wa nchi hiyo, walitekeleza mpango wa uhamasishaji uchumi na hayati Rais Mwai Kibaki ili kukuza uchumi na kusababisha uchumi wa Kenya kutoka katika mdororo.

"Tunajua kuendesha uchumi. Tuliingia kwa serikali kama uchumi ilikua imeathirika na mbaya  kuliko hapa," Raila alisema.

Alisema miongoni mwa mawazo yao ni kuanzishwa kwa elimu ya msingi bila malipo ambayo walihakikisha inatekelezwa bila kukosa kama walivyoahidi wakati wa kampeni za Narc.

Raila alisema kwa sababu ya kuanzishwa kwa elimu bila malipo, shule zilijaa kiasi kwamba wanafunzi walilazimika kujifunzia chini ya miti na wengine katika madarasa ya kubahatisha kwenye mahema.

Ruto ameendelea kushinikiza kupitishwa kwa Mswada wa Fedha huku kukiwa na upinzani mkali kutoka kwa viongozi wa kisiasa, makasisi na mashirika mbalimbali.

Muswada huo unaolenga kupanua wigo wa kodi na kuongeza ukusanyaji wa mapato una mapendekezo ya kodi yenye utata ikiwa ni pamoja na tozo ya lazima ya asilimia tatu kwa Mfuko wa Nyumba.

Azimio chini ya uongozi wa Raila alitaja hatua hizo kuwa "daraja kuu katika kumfanya kila Mkenya awe mnyonge."

Raila mnamo Jumanne alifanya mkutano wa Kundi la Wabunge jijini Nairobi ili kutoa njia mbele baada ya mazungumzo ya pande mbili ambayo yalilenga kutatua masuala tata kuhusu Mswada huo na masuala ya uchaguzi kugonga mwamba wiki jana.