Kisii: Waandamanaji wawasha moto huku polisi wakitumia vitoa machozi kuwatawanya

Waandamanaji hao walisema hawakufurahishwa na kupanda kwa gharama ya maisha.

Muhtasari

•Polisi wa kutuliza ghasia wakiongozwa na kamanda wa kaunti Charles Kasses walilazimika kutumia vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji.

Waandamanaji waliwasha moto huko Kisii mnamo siku ya Ijumaa,7, Julai
Waandamanaji waliwasha moto huko Kisii mnamo siku ya Ijumaa,7, Julai

Waandamanaji mjini Kisii walimiminika mitaani kulalamikia gharama ya juu ya maisha siku ya Ijumaa.

Vijana waliwasha matairi kwenye barabara na kukimbizana na polisi. Kando ya barabara za Kisii-Kilgoris, mioto ilikuwa imewashwa.

Polisi wa kutuliza ghasia wakiongozwa na kamanda wa kaunti Charles Kasses walilazimika kutumia vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji.

Katika baadhi ya matukio, polisi walilazimika kurudi nyuma walipozidiwa na waandamanaji.

Katika baadhi ya matukio, waliwalazisha polisi kurudi nyuma
Katika baadhi ya matukio, waliwalazisha polisi kurudi nyuma
Image: Magati Obebo

Matukio sawia yalishuhudiwa kando mwa barabara ya Kisii-Keroka ambapo vijana walifunga barabara.

Waliohutubia wanahabari walisema hawakufurahishwa na kupanda kwa gharama ya maisha.

"Serikali hii iteka imani ya watu kushinda lakini sasa inatutoza ushuru dhalilishi," Manases Austin alisema.

Maandamano hayo, alisema, yataendelea hadi Rais William Ruto achukue hatua ya kudhibiti gharama ya maisha.

Daniel Nyabwari, ambaye pia alishiriki maandamano, alisema hakuna aliyelipwa kujiunga na maandamano hayo. 

"Sote tumefika hapa kwa sababu tuna hasira na serikali, gharama ya kila kitu cha msingi inagonga paa lakini wenye mamlaka wanajitenga na kutengwa na maumivu tunayopitia," alisema.

"Alisisitiza kupunguzwa kwa bei ya mafuta akisema gharama kubwa ya maisha mahali popote ni kichocheo cha rabsha."

Joseph Obwoge, alipuuzilia mbali dhana kwamba wakazi wa Kisii hawana shida na gharama za chakula.

"Wale wanaouza simulizi kuwa Kisii haina shida na chakula ni wabinafsi, tunawafahamu. Tumeathirika kama Wakenya wengine," akasema.

Wakati huo huo, doria za usalama ziliimarishwa haswa katikati mwa mji wa Kisii ili kuvuruga  maonyesho ya Kilimo yanayoendelea.