Maandamano ya Saba Saba yazidi kushika kasi kote nchini

Serikali imeimarisha usalama kote nchini hasa katika kaunti zinazoaminika kuwa maeneo ya ghasia.

Muhtasari

• Raila Odinga anatarajiwa kuongoza mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kamukunji kuzindua zoezi la kukusanya saini na pengine awamu ya pili ya maandamano ya kuipinga serikali.

•Waandamanaji hao Waliiomba serikali kupunguza gharama za maisha.

Waandamani wakati wa maandamano ya saba saba.
Waandamani wakati wa maandamano ya saba saba.
Image: DANIEL OGENDO

Maandamano ya Saba Saba yanayoongozwa na muungano wa Azimio yanazidi kushika kasi kote nchini. Maandamano hayo, katika video zilizoonekana na Radio Jambo, yalianza mapema saa tatu asubuhi siku ya Ijumaa.

Huku maandamano hayo yakiongozwa kwa kiasi kikubwa na upinzani, makundi ya kutetea haki za kibinadamu yamejiunga kupinga hatua ya serikali ya Kenya kwanza kupitisha sheira ya Fedha ya mwaka 2023.

Katika baadhi ya maeneo ya jiji la Nairobi, kundi la waandamanaji lilionekana karibu na hoteli ya zamani ya Hilton.

Waandamanaji hao Waliiomba serikali kupunguza gharama za maisha.

Aidha watu kathaa watu kadhaa wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Mjini Kisumu, barabara zimefungwa na moto kuwashwa huku wenyeji wakiingia mitaani kuitikia wito wa kiongozi wa Azimio Raila Odinga wa kuandamana. Polisi kwa sasa wanakita kambi  katika maeneo tofauti ndani ya mji huo.

Mjini Mombasa, wanaharakati na wakazi pia waliingia mitaani mapema kuandamana kupinga gharama ya juu ya maisha. Hata hivyo, polisi walilazimika kutumia vitoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji hao.

Mapema Ijumaa, ripoti zilisema kuwa kundi la vijana katika eneo la Mathare lilifunga barabara kuu ya Thika na walikuwa wakiyapiga magari mawe.Video zilizosambaa kwenye mtandao wa Twitter zilionyesha magari kadhaa yakirudi walipotoka.

Hata hivyo, polisi walifika kwa wakati na kuwatawanya vijana.

Serikali imeimarisha usalama kote nchini na kaunti zinazoaminika kuwa maeneo ya ghasia.

Raila Odinga anatarajiwa kuongoza mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kamukunji kuzindua zoezi la kukusanya saini na pengine awamu ya pili ya maandamano ya kuipinga serikali.

Viongozi wenza wa Azimio pia watazindua maandamano katika maeneo mengine ya nchi.

Hii ni sehemu ya mkakati wa upinzani wa kutaka wafuasi wake wajiandae na upinzani kutoka mashinani na kuongeza shinikizo lao dhidi ya utawala wa Rais William Ruto.

Katika mpango wa Azimio, baada ya mkutano wa Raila katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji jijini Nairobi, waandamanaji wataandamana hadi katikati ya jiji la Nairobi.

Wafuasi wa Azimio wanatarajiwa kukusanyika katika maeneo mawili jijini Nairobi, ikiwa ni pamoja na Kamukunji na Kibera kabla ya kuandamana kuelekea CBD.

Huko Ukambani, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka atafanya mkutano wa kuipinga serikali katika eneo la Kathiani, Kaunti ya Machakos.