Familia iliyopoteza watu 7 katika ajali ya Makindu yaomba msaada wa Ksh 4M kwa ajili ya mazishi

“Mzigo huu si rahisi, maana mara nyingi tunaongea kuhusu: tunazika, tuna jeneza, tuna maua, tuna hearse… sasa tunaongea mara 7. Tulikuwa tunaongea mara 6 sasa ni mara 7. You can imagine.”

Muhtasari

• Mwaniki alisonga mbele na kuorodhesha jinsi bajeti hiyo ya shilingi milioni 4 itakavyotumika katika kuandaa mazishi ya wanafamilia hao 7.

• “Tulifanya makadirio yetu na tukaona ya kwamba pengine, kando na zile running costs za kila siku, tunahitaji karibu milioni 4." alisema Mwaniki.

Image: George Owiti

Familia moja kutoka kaunti ya Nakuru ambayo ilipoteza wanafamilia Zaidi ya 5 katika ajali mbaya katika barabara kuu ya Mombasa- Nairobi eneo la Salama wakati wa mtoko wa Pasaka imeomba msaada wa Zaidi ya milioni 4 kwa ajili ya mipango ya mazishi.

Familia hiyo kupitia kwa msemaji wao kwa jina Mwaniki waliweka wazi bajeti hiyo nzito katika ibada ya wafu iliyoandaliwa jioni ya Jumapili na kupeperushwa moja kwa moja kwenye chaneli ya YouTube ya mhisani Karangu Muraya.

Ripoti za awali zilisema kwamba familia hiyo ilipoteza jumla ya watu 6 lakini msemaji wa familia alisema kwamba mtu mmoja Zaidi alifariki baadae hospitalini na kuifanya idadi jumla ya wanafamilia waliokufa kwenye ajali kuwa watu 7.

“Haya yametupata, kwa hivyo sisi hatuna la kusema wala kumlaumu Mungu wala mtu yeyote maana haya mambo yanapofanyika kuna zile dhana watu husema lakini sisi tumesimama na kauli mbiu kwamba Mungu ni mwema,” Mwaniki alianza.

“Hiyo ndio kauli mbiu yetu, ya kwamba, licha ya haya mambo yote kufanyika, maana kuwapoteza wapendwa 6, na leo hii asubuhi ya leo yule ambaye alikuwa kwenye ICU, ametuacha. Yule mdogo ambaye alikuwa hospitali ya Karen, sasa tutaongeza pia picha yake kwenye bango hilo lenye wanafamilia 6 tayari marehemu,” aliongeza kwa huzuni.

Mwaniki alisonga mbele na kuorodhesha jinsi bajeti hiyo ya shilingi milioni 4 itakavyotumika katika kuandaa mazishi ya wanafamilia hao 7.

“Mzigo huu si rahisi, maana mara nyingi tunaongea kuhusu: tunazika, tuna jeneza, tuna maua, tuna hearse… sasa tunaongea mara 7. Tulikuwa tunaongea mara 6 sasa ni mara 7. You can imagine.”

“Halafu siku hiyo ndio tuwatoe kule Makindu na Salama, ambelensi zilikuwa zinakimbia kila sehemu na wakati huo ndio nilijua kwamba ukiona ambulensi inapiga king’ora, ujue kuna pesa zinatumika hapo, kando na kuipisha ipite… wakati huo ndio tulijua kwamba ambulensi sio matatu kuabiri tu kwa shilingi 200-300,” alisema.

“Tulifanya makadirio yetu na tukaona ya kwamba pengine, kando na zile running costs za kila siku, tunahitaji karibu milioni 4. Hiyo ni kabla hatujahesabu yale yamejiri siku ya leo na yale yatakayotokea siku zijazo,” Mwaniki alimaliza.