Mshukiwa akamatwa na bangi ya thamani ya Sh600,000

Mwanaume huyo alikuwa anaelekea eneo la Kiaruguru,kaunti ndogo ya Ruiru

Muhtasari

•Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) katika taarifa Alhamisi ilisema mshukiwa alikamatwa kando ya barabara ya  Eastern Bypass.
•Kukamatwa kwa mtu huyo kunafuatia taarifa za kijasusi, ambazo zilisababisha kukamatwa kwa gari alilokuwa akiendesha.

Pingu

Polisi jijini Nairobi wanamshikilia mwanamume mmoja kwa tuhuma za ulanguzi wa mihadarati.

Idara ya upelelezi wa jinai (DCI) katika taarifa Alhamisi ilisema mshukiwa alikamatwa kwenye barabara ya  Eastern Bypass. DCI ilisema bangi ambayo thamani yake ya mtaani inakadiriwa kuwa Sh600,000 ilipatikana wakati wa operesheni hiyo.

Kulingana na DCI, kukamatwa huko kunafuatia maafisa wa kijasusi, ambao walisababisha kukamatwa kwa gari alilokuwa akiendesha mwanamume huyo na kikosi cha kupambana na mihadarati.

"Mmea ambao ulikuwa umefichwa kwenye mfuko wa gunia ndani ya  marobota manne na gari umezuiliwa kama vielelezo vinavyosubiri kufikishwa mahakamani kwa mshukiwa," DCI ilisema.

Mshukiwa huyo kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha polisi jijini Nairobi. Haya yanajiri takriban wiki tatu baada ya maafisa wa polisi kutoka kitengo cha kupambana na mihadarati kunasa magunia saba ya bangi mjini Kilifi.

Bangi hiyo ilikuwa na uzito wa kilo 429.3 na ilikuwa na thamani ya mtaani ya Sh12,879,000.Afisa wa uchunguzi wa jinai katika kaunti ya Kilifi David Sielle alisema bangi hiyo ilinaswa katika eneo la Kibao Kiche kando ya barabara kuu ya Mariakani Mavueni. CCIO ilisema bangi hiyo ilipakiwa kwenye lori  na washukiwa wawili kukamatwa.