Mbunge Peter Salasya hatimaye akutana na mwanadada aliyeomba kuwa mke wake

Bi Lydia Ronald alitumia bango kukiri mapenzi yake makubwa kwa Salasya.

Muhtasari

•Siku ya Jumanne mbunge huyo alipakia video iliyoonyesha akiwa kwenye kikao na mwanadada huyo huko bungeni.

•Alidokeza kuwa rais Ruto alikuwa amempa changamoto la kutafuta mke kuona bado hayupo kwenye ndoa.

akutana na Lydia Ronald katika bunge siku ya Jumanne.
Mbunge wa Mumias East Peter Salasya akutana na Lydia Ronald katika bunge siku ya Jumanne.
Image: TWITTER// PETER SALASYA

Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Kalerwa Salasya hatimaye ametimiza ahadi aliyotoa siku chache zilizopita ya kumwalika Bi Lydia Ronald kwenye  bunge la kitaifa kwa ajili ya chakula cha mchana.

Bi Lydia ni mwanadada ambaye alionekana kwenye video iliyosambaa mitandaoni mapema wiki jana  akiwa ameiunua bango lililokuwa na maandishi ya ombi  la ndoa kwa mbunge huyo wa mara ya kwanza.

Katika bango hilo, alijitambulisha kama mwanamke mcha Mungu, mwenye bidii  na mnyenyekevu ambaye angeweza kuwa mke kamili wa Salasya.

"Mbunge Peter Salasya, nioe tafadhali. Mheshimiwa wa Mumias. Mimi ni Lydia Ronald," bango hilo lilisoma.

Lydia pia aliandika namba yake ya simu kwenye bango hilo ambalo alionekana nalo katika eneo la Archives, jijini Nairobi.

“Ninamuahidi kwamba akinichagua kuwa mke wake sitamkatisha tamaa,” alisikika akisema katika video hiyo.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Mbunge Salasya alimjibu mwanamke huyo kwa utani na kumtafuta kwa simu.

Alidokeza kuwa rais Ruto alikuwa amempa changamoto la kutafuta mke kuona bado hayupo kwenye ndoa.

"Warembo na Salasya nawapenda sana .Nitakufikia na kukusalimia. Rais William Ruto nakumbuka uliniuliza kama nimepata mke  sasa ulipotutembelea katika Bunge la Taifa, naona mambo si mbaya vile kunaenda. Mungu ibariki kenya.Nchi yetu imebarikiwa," alisema.

Siku ya Jumanne mbunge huyo alipakia video iliyoonyesha akiwa kwenye kikao na mwanadada huyo huko bungeni.

Salasya alimlimbikizia Lydia sifa kemkem na kudokeza azma yake ya siasa huku akimtabiria mafanikio makubwa.

"Lydia atakuwa mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Kisii au kumrithi rafiki yangu Sylvanus Osoro, Mbunge wa Mugirango Kusini. Ujasiri wake na ushawishi itachukua mahali pake," alisema kupitia Twitter.

Salasya ni miongoni mwa wabunge wadogo zaidi ambao walichaguliwa katika uchaguzi wa Agosti 9.

akutana na Lydia Ronald katika bunge siku ya Jumanne.
Mbunge wa Mumias East Peter Salasya akutana na Lydia Ronald katika bunge siku ya Jumanne.
Image: TWITTER// PETER SALASYA