Mwanawe Museveni atangaza azma ya kuwania urais wa Uganda

Muhoozi alieleza imani yake kuwa wananchi wa Uganda watamuunga mkono na kumpigia kura.

Muhtasari

•"Njia pekee ya kumlipa mama yangu ni kuwa Rais wa Uganda! Na kwa uhakika nitafanya hivyo!!" Muhoozi alisema.

•Wengine walimpinga na kumwambia kuwa hatafaulu kupata uongozi wa nchi hiyo hata ifanyike nini.

KWA HISANI
KWA HISANI
Image: Muhoozi Kainerugaba

Jenerali mkuu wa majeshi ya Uganda, Muhoozi Kainerugaba ambaye pia ni mtoto wa rais wa Uganda Yoweri Museveni ametangaza azma yake ya kuwa rais wa nchi hiyo.

Muhoozi amedokeza kuwa atawania kiti cha urais katika siku za usoni na kueleza imani yake kuwa wananchi wa Uganda watamuunga mkono na kumpigia kura.

"Njia pekee ya kumlipa mama yangu ni kuwa Rais wa Uganda! Na kwa uhakika nitafanya hivyo!!" Muhoozi alisema kwenye Twitter.

Baadhi ya wafuasi wake Waganda walikubaliana naye na kumshauri awanie kiti hicho cha juu zaidi baada ya baba yake kustaafu.

Baadhi ya majibu:

"Endelea na uamuzi wako ndugu, ndoto zako zitatimia. Wewe ni kiongozi mdogo ila una maono ya nchi hii, si kama Bobi Wine ambaye azimio lake ni kumtoa Museveni uongozini!" Ukambani UDA King alisema.

" Jenerali anapendwa na kuungwa mkono na mamilioni ya vijana ambao ni wengi kupita kiasi kinachohitajika," MR.JORDAN alisema na kuchapisha video iliyoonyesha wafuasi wengi wakimshangilia Muhoozi.

Hata hivyo wengine walimpinga na kumwambia kuwa hatafaulu kupata uongozi wa nchi hiyo hata ifanyike nini.

"Unafahamu vyema kuwa huna mahali popote huku Uganda na rohoni mwako unajua kuwa huna mapendeleo yoyote kutoka kwa wananchi wa Uganda. Najua kuna wakati ambao Waganda watachagua viongozi wanaotaka ila si kwa mtutu wa bunduki,"  Hon James Mubiru aliandika.

"Ukiwa na umri wako wa miaka 50, baba yako hakuaminii na simu, unataka Waganda wakuamini na nchi?!Jenerali mkuu tulia na ujinyakulie chupa nyingine," NUP FOREVER aliandika.

Hivi majuzi, Jenerali huyo alikuwa ameonya chama cha upinzani cha Uganda  kuwa bado atashinda viongozi wao na kujinyakulia kiti cha urais baada ya baba yake.

"Kwa wanachama wa upinzani, baada ya baba yangu, nitawashinda katika uchaguzi wowote ule. Waganda wananipenda kuliko wanavyowapenda nyinyi," Muhoozi alisema.