Wacha kuota Raila kila wakati hata ukiwa na mkeo - Orengo amwambia DP Gachagua

Badala yake wafanyie wananchi Kazi waliwapatia - Orengo alimwambia.

Muhtasari

• Ndoto ambazo anaota ni Raila, Raila. Awache kusumbua mama watoto na Raila Raila hata kama amelala - Orengo alimsuta DP Gachagua.

Seneta wa Siaya James Orengo
Seneta wa Siaya James Orengo
Image: STAR

Gavana wa Siaya James Orengo amemjia juu naibu rais Rigathi Gachagua kwa kile alisema kwamba anamtaja kinara wa ODM Raila Odinga kila wakati bila maana yoyote.

Orengo ambaye alikuwa anazungumza Jumatatu, siku moja baada ya DP Gachagua kumkandia vikali Odinga, alimtaka kuliondoa kabisa jina la mwanasiasa huyo kongwe kinywani mwake.

“Na Rigathi amezoea kuzungumzia Raila kila mahali, sijui kama analala usiku karibu na mama. Ndoto ambazo anaota ni Raila, Raila. Awache kusumbua mama watoto na Raila Raila hata kama amelala. Badala yake wafanyie wananchi Kazi walipatiwa. Mimi nauliza, fanyeni kazi na muache kulia kuwa Uhuru alifanya hii Raila alifanya hii, ni nyinyi sasa mlioko na jukumu la kutekeleza,” Orengo alisema.

Orengo alisema kwamba wao kama upinzani wanapenda kuifanya kazi yako kama wapinzani na kuwa hawatoisaza serikali ya Kenya Kwanza oindi itakapofeli kutekeleza manifesto na ahadi walizozitoa kwa wananchi.

“Mkikosa, kama mmeanza kukosa namna hii, hatutaweza kuangalia nyuma. Sisi tuko bado na chuma kile cha zamani na moto utawaka hapa Kenya mkifanya porojo ya kutofanya kazi jinsi mliahidi Wakenya,” Orengo alitoa tahadhari.

Jumapili katika hafla moja ya kanisa naibu rais Rigathi Gachagua alimkujia juu Raila odinga huku akimtaka kuwakoma na kuwaacha wafanye kazi kwani hawana haja na yeye.

“Hatukutafuti, na hatuna wakati; mara ya mwisho ulipoingia kwenye serikali ya Uhuru uliiharibu. Acha kusema watu wanaweza kukulazimisha uje kwenye serikali hii. Hatutaki usaidizi wa mtu yeyote,” Gachagua alisema kwa ukali.