Muhula wa urais upunguzwe hadi miaka 3 au 4 - Okiya Omtatah anguruma

Hii ni baada ya mbunge wa Fafi kusema ana mswada wa kurekebisha katiba ili kuondoa ukomo wa mihula ya urais

Muhtasari

• Baadhi yetu tunadhani tupunguze ukomo wa muda hadi miaka mitatu au minne. - Omtatah.

Omtatah apinga vikali pendekezo la kuondoa ukomo wa urais
Omtatah apinga vikali pendekezo la kuondoa ukomo wa urais
Image: Screengrab//CitizenTV

Seneta wa Busia Okiya Omtatah amejiunga kwenye mazungumzo kuhusu ukomo wa muhula wa urais, ambao baadhi ya wabunge wanataka kutupiliwa mbali.

Akizungumza Jumanne usiku kwenye mahojiano na runinga ya Citizen, saa chache baada ya mbunge wa Fafi, Salah Yakub kudai kuwa ana pendekezo la kutaka ukomo wa mihula miwili kwa uongozi wa rais kuondolewa na badala yake kubadilishwa na umri wa miaka 75 kuwa kigezo muhimu katika mtu wa kuwania urais, Omtatah alisema yeye anataka kipengele hicho kipunguzwe hadi miaka hata kama ni mihula miwili lakini kila muhula na miaka iliyopungua.

“Baadhi yetu tunadhani tupunguze ukomo wa muda hadi miaka mitatu au minne. Mihula miwili lakini muda mfupi kuliko miaka kumi. Ili ikiwa mtu anafanya makosa, tunaweza kuyaondoa mapema zaidi. Wazo kwamba tunaweza kuongeza muda wa mtendaji mkuu kwangu ni jambo ambalo sielewi linapotoka,”

Omtatah alisema atakuwa mstari wa mbele kupinga njama hizo za kuongeza muda wa rais kutoka miaka kumi ya kikatiba.

“Baadhi yetu tuko tayari kupigana nayo. Sijui kama tutafaulu, lakini kutakuwa na vita. Na itakuwa mbaya. Uadilifu na usafi wa siasa zetu ni katika kubadilisha wanasiasa jinsi tunavyobadilisha nepi kwa mtoto,” Omtatah alisema.

 Kama ilivyo sasa hivi nchini Kenya, rais anaruhusiwa kuongoza kwa mihula miwili tu ambayo inagawanyika kwa miaka mitano kila muhula.

Mbunge wa Fafi alizua tafrani miongoni mamilioni ya Wakenya baada ya kudai kwamba atawasilisha mswada bungeni wa kutaka kurekebishwa kwa kipengele cha katiba kinachotaka rais kuongoza kwa mihula miwili tu na badala yake kuruhusiwa kusalia madarakani mpaka anapofikisha miaka 75.