Sakaja aguswa moyo na mtoto wa mtaani, aahidi kufadhili elimu yake

Sakaja alifichua kuwa kijana huyo sasa ana familia na ataenda shuleni

Muhtasari

• Gavana huyo alimpeleka Ibrahim kwenye ofisi yake ambapo kijana huyo alikuwa na muonekano mpya.Alikuwa amevaa nguo mpya na hata kunyolewa nywele.

GAVANA WA NAIROBI JOHNSON SAKAJA
Image: SAKAJA/TWITTER

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja amemfariji kijana mmoja ambaye hana familia na amekuwa akiishi kwenye mitaa ya Nairobi.

Sakaja alikuwa kwenye ziara yake katika mji wa Nairobi Jumanne ndipo akakutana na kijana huyo.

"Ibrahim Ali. Kijana huyu alinigusa moyo. Wakati wa kukagua kazi zinazoendelea katika CBD, alikuja kwangu na kusema anataka kuenda shule. Amekuwa akiishi mtaani kwa miezi kadhaa baada ya kutelekezwa," Sakaja alisema.

Sakaja alifichua kuwa aliamua kumchukua mtoto huyo na kumtoa kwenye mitaa ya Nairobi ili awe na familia.

Alisema kuwa ana imani kuwa mtoto huyo atakuwa na mafanikio kwenye siku za usoni.

Gavana huyo alimpeleka Ibrahim kwenye ofisi yake ambapo kijana huyo alikuwa na muonekano mpya.Alikuwa amevaa nguo mpya na hata kunyolewa nywele.

Sakaja amekuwa akionyesha juhudi za kutaka kuwasaidia vijana wa mji wa Nairobi kutoka pale alipochaguliwa.

Hivi majuzi alisema kuwa vijana watapewa kazi angalau kama ya kupanda miti kisha kulipwa Shillingi 2500 ili kuweza kujikimu.

Amekuwa pia akiwahimiza vijana kuepuka na mambo ya kihalifu kama kuwaibia watu, jambo ambalo limekuwa likiwakwaza wakaazi wa mji wa Nairobi kwa muda sasa.

"Vijana, uhalifu sio mzuri, hata kama mna shida kiasi gani, mtupe wakati. Mlitupa kazi, tutawashikilia na kuwapa kazi. Ila mkishikwa msinipigie," Sakaja alisema.