"Ni uongo!" Modern Coast wakanusha taarifa za kifo katika ajali ya basi lao Kisii

Abiria wote 43 waliokuwemo ndani ya basi hilo walishuka salama na baadhi wakiwa na majeraha madogo.

Muhtasari

• Walisema kuwa abiria wengi hawakuumia ila waliendelea na safari kutumia basi lingine ambalo lilifika hapo.

• Awali taarifa kutoka kwa mashuhuda zilisema kuwa mtu mmoja alipoteza maisha katika ajali hiyo baada ya basi kutumbukia mtoni kando ya barabara.

Basi la Modern Coast lililofanya ajali Kisii
Basi la Modern Coast lililofanya ajali Kisii
Image: Facebook

Kampuni ya usafiri ya Modern Coast imejitokeza wazi na kutoa taarifa kuhusu ajali ya moja ya basi lao lililoanguka katika kaunti ya Kisii asubuhi ya Jumatano.

Awali taarifa kutoka kwa walioshuhudia ajali hiyo Kisii walisema kuwa dereva wa basi hilo alipoteza mwelekeo alipokuwa akijaribu kukwepa mtu aliyekuwa akivuka barabara na hivyo ndivyo basi lilijipata limetumbukia katika mto kando ya barabara viungani mwa mji wa Kisii.

Taarifa zilidai kuwa mtu mmoja aliyegongwa na basi hilo alipoteza maisha lakini kampuni ya Modern Coast imekanusha madai hayo na kusema kuwa taarifa zinazosambazwa mitandaoni ni za kupotosha kwani hakuna mtu aliyefariki katika ajali hiyo ya mapema Jumatano.

Japo walidhibitisha kisa cha ajali hiyo na kusema kuwa baso lao liligonga gari la matatu ndogo kabla ya kutumbukia mtoni, walikanusha kutokea kwa vifo bali ni abiria waliojeruhiwa na ambao wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali mbalimbali mjini Kisii.

“Leo basi letu kutoka Mombasa kuelekea Homabay likiwa linarudi nyuma kwenye barabara ya Maraam huko Kisii ili kuegeshwa kwa mteremko, liligonga matatu. Matokeo yake dereva aliingiwa na hofu na basi likateleza na kuanguka ubavu kwenye shimo. Abiria wote 43 waliokuwemo ndani ya basi hilo walishuka salama na baadhi wakiwa na majeraha madogo walipelekwa kwa matibabu huku wengine wakiendelea na safari na basi lingine. Kinyume na taarifa zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii, hakukuwa na majeruhi wa abiria,” taarifa hiyo ilisoma kwa ukamilifu.