Huduma za Modern Coast zasimamishwa mara moja kufuatia ajali iliyoua watu 33

Watu 33 walithibitishwa kufariki huku wengine kumi wakiendelea kupokea matibabu kufuatia ajali hiyo.

Muhtasari

•NTSA  imetangaza kusimamishwa kwa huduma za Modern Coast na kusema uchunguzi kuhusiana na ajali hiyo unaendelea.

•NTSA ilisema huduma za kampuni ya Modern Coast zimesimamishwa katika njia zake zote hapa nchini.

Basi la Modern Coast latumbukia kwenye mto Nithi
Image: HISANI

Huduma za kampuni ya Modern Coast  Express Limited zimesimamishwa kufuatia ajali mbaya iliyotokea Jumapili jioni na kupelekea vifo vya watu 33.

Jumapili mwendo wa saa kumi na mbili unusu, basi la Modern Coast ambalo lilikuwa likisafirisha abiria kutoka Meru kuelekea Mombasa lilipoteza mwelekeo na kutumbukia ndani ya mto Nithi.

Kufikia Jumatatu asubuhi, watu 33 walithibitishwa kufariki huku wengine kumi wakiendelea kupokea matibabu maalum kufuati ajali hiyo.

NTSA sasa imetangaza kusimamishwa kwa huduma za kampuni hiyo na kusema uchunguzi kuhusiana na ajali hiyo unaendelea.

"Uchunguzi wa kina wa mashirika mengi kuhusu ajali hiyo na tathmini ya viwango vya uendeshaji wa usalama wa mtoa huduma unaendelea kwa sasa. Tunatoa pole kwa familia za waliopoteza wapendwa wao katika ajali hii mbaya na tunawatakia afueni ya haraka waliopatiwa matibabu," Taarifa ya NTSA ilisoma.

NTSA ilisema huduma za kampuni ya Modern Coast zimesimamishwa katika njia zake zote hapa nchini.

Njia hizo ni pamoja na; Nairobi-Mombasa, Nairobi-Thika-Embu-Meru-Maua, Mombasa-Makindu-Wote-Kitui-Machakos na njia za Nairobi-Narok-Kisii-Homa Bay-Migori-Isibania.

Hakuna basi lolote la kampuni hiyo ambalo litaruhusiwa barabarani kufuatia hatua hiyo. Kwa sasa kampuni ya Modern Coast ina mabasi  yanayosafirisha abiria katika njia mbalimbali za Kenya.

Basi lililohusika kwenye ajali Jumapili Inaripotiwa kupoteza mwelekeo na kuacha  barabara baada ya breki zake kushindwa kufanya kazi. Basi hilo lilianguka umbali wa futi 40 hadi kwenye mto Nithi.

Maafisa wa polisi walifika kwenye eneo la tukio kuwasaidia raia katika shughuli ya kuopoa miili na kuokoa majeruhi kutoka kwa mabaki  ya basi hiyo.

Majeruhi walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Chuka na Hospitali ya Misheni ya PCEA Chogoria.