Idadi ya watu waliofariki katika ajali ya basi huko Tharaka Nithi yafikia 33

Basi la Modern Coast lilitumbukia mtoni kando ya barabara kuu ya Meru - Mombasa.

Muhtasari

•Kamishna wa Mkoa wa Mashariki Evans Achoki alisema Jumatatu asubuhi kwamba vifo vimeongezeka hadi 33.

•Shirika la Msalaba Mwekundu Jumapili liliweza kuwaokoa baadhi ya waathiriwa, ambao walikimbizwa hospitalini.

Basi la Modern Coast latumbukia kwenye mto Nithi
Image: HISANI

Takriban watu 33 wamefariki baada ya basi kutumbukia mto Nithi kaunti ya Tharaka Nithi siku ya Jumapili.

Dereva wa basi la Modern Coast alipoteza udhibiti wa gari hilo, na kutumbukia mtoni kando ya barabara kuu ya Meru - Mombasa.

Kamishna wa Mkoa wa Mashariki Evans Achoki alisema Jumatatu asubuhi kwamba vifo vimeongezeka hadi 33.

Walioshuhudia walisema kuwa basi hilo lililokuwa likielekea Mombasa lilikuwa likisafiri kutoka Meru Mjini wakati ajali hiyo ilipotokea.

Shirika la Msalaba Mwekundu Jumapili liliweza kuwaokoa baadhi ya waathiriwa, ambao walikimbizwa hospitalini.

Ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa kumi na mbili jioni.

Majeruhi walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Chuka na Hospitali ya Misheni ya PCEA Chogoria.

Ajali hiyo ilitokea mwezi mmoja tu baada ya Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) kutoa ripoti kuhusu kuongezeka kwa idadi ya vifo kufuatia ajali za barabarani.

Kulingana na NTSA, takriban 2,211 wamefariki kwenye barabara za Kenya kati ya Januari na Juni mwaka huu, ikilinganishwa na 1,988 waliofariki wakati huohuo mwaka wa 2021.

Waendesha pikipiki 608 walikufa katika kipindi kama hicho mwaka huu ikilinganishwa na 569 mnamo 2021, wakati abiria 362 walikufa katika miezi sita iliyopita ikilinganishwa na 326 mnamo 2021.

Idadi ya madereva waliofariki kutokana na ajali ilisalia kuwa 210.

Watembea kwa miguu 788 walifariki kati ya Januari na Juni mwaka huu ikilinganishwa na 651 mwaka jana.

Abiria waliofariki wameongezeka hadi 211 ikilinganishwa na 182 waliofariki mwaka 2021.

Waendesha baiskeli 32 walifariki katika kipindi hicho ikilinganishwa na 50 walioangamia mwaka jana.

Kwa mujibu wa polisi, Mwendo kasi umekuwa chanzo kikuu cha ajali hizo.

Kuendesha gari kiholela, kupita magari kihatari, kuendesha gari ukiwa mlevi, kutembea ukiwa mlevi, kuendesha pikipiki/baiskeli ukiwa mlevi, na kushindwa kutumia helmeti miongoni mwa masuala mengine pia yamehusishwa na ongezeko la ajali.

(Utafsiri: Samuel Maina)