Takriban watu 20 wafariki baada ya basi kutumbukia ndani ya mto Nithi

Basi hilo lilianguka umbali wa futi 40 hadi kwenye mto Nithi.

Muhtasari

•Basi hilo lilikuwa likisafirisha abiria kutoka Meru hadi Mombasa wakati lilipohusika kwenye ajali hiyo.

•Basi hilo lilipoteza mwelekeo na kuacha  barabara kuu ya Meru-Mombasa baada ya breki zake kushindwa kufanya kazi.

Basi la Modern Coast latumbukia kwenye mto Nithi
Image: HISANI

Takriban watu 21 wamethibitishwa kufariki baada ya basi la kampuni ya Modern Coast kutumbukia katika mto Nithi kaunti ya Tharaka Nithi siku ya Jumapili.

Basi hilo lilikuwa likisafirisha abiria kutoka Meru hadi Mombasa wakati lilipohusika kwenye ajali hiyo mwendo wa saa kumi na mbili  unusu jioni.

Inaripotiwa kwamba basi hilo lilipoteza mwelekeo na kuacha  barabara baada ya breki zake kushindwa kufanya kazi. Basi hilo lilianguka umbali wa futi 40 hadi kwenye mto Nithi.

Maafisa wa polisi walifika kwenye eneo la tukio kuwasaidia raia katika shughuli ya kuopoa miili na kuokoa majeruhi kutoka kwa mabaki  ya basi hiyo.

Polisi, kikosi cha Zimamoto  cha kaunti ya Tharaka Nithi na wananchi walisaidia katika shughuli za uokoaji.

Kulingana na  taarifa ya Huduma ya Msalaba Mwekundu, juhudi za uokoaji  zilisitishwa kutokana na giza.

Majeruhi walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Chuka na Hospitali ya Misheni ya PCEA Chogoria.

Nicholas Mutegi, mmoja wa walioshuhudia alisema basi hilo lilikuwa likishuka kwa kasi kwenye mteremko mkali wa Nithi kabla ya ajali hiyo kutokea.

"Iligonga reli za walinzi na kuanguka ndani ya maji. Nilisikia kishindo kikubwa kilipoanguka umbali wa mita 40 na kusababisha basi kuwa mabaki. Niliweza kuhesabu zaidi ya maiti 10 zilizowekwa kwenye gari la polisi na zaidi ya 20 kujeruhiwa," Mutegi alisema.

Haya yanajiri takriban mwezi mmoja tu baada ya matatu ya abiria 14 kuanguka kutoka kwa daraja ya Nithi na kuua abiria mmoja huku wengine 13 wakijeruhiwa vibaya.