Mathare: Kundi la kina mama wapiga magoti mbele ya polisi wakiomba kusitishwa kwa vurugu

Kina mama hao waliwaomba polisi kuacha kutupa vitoa machozi kwani kufanya hivyo ni kuwachochea vijana kujibu kwa mawe.

Muhtasari

• Kina mama hao walijitokeza wakiwa wameinua mikono juu kama njia moja ya kujisalimisha kwa polisi wakiwa na ombi kwao.

Kundi la kina mama wakipiga magoti mbele ya polisi
Kundi la kina mama wakipiga magoti mbele ya polisi
Image: Screengrab

Tukio la kupendeza na ambalo si la kawaida limeshuhudiwa katika mtaa wa mabanda wa Mathare jijini Nairobi, adhuhuri ya Alhamisi wakati wa makabiliano baina ya maafisa wa polisi na waandamanaji.

Tukio hilo ambalo lilionekana kwenye runinga ni pale ambapo kundi la kina mama walijitokeza wakiwa wameinua mikono yao juu kama njia moja ya kujisalimisha mbele ya maafisa wa polisi.

Kina mama hao walijongea mbele ya kundi la maafisa wa polisi wakiwa na rungu pamoja na vitoa machozi na bunduki mikononi mwao, na lengo lao lilikuwa ni kutoa ombi la ukweli kwa polisi kusitisha vuta nikuvuta baina yao na polisi.

Kina mama wapiga magoti mathare
Kina mama wapiga magoti mathare

Kina mama hao ambao wanaonekana katika hali ya kutia huruma waliinua mikono yao juu na kupiga magoti wakiwaomba polisi kusitisha kuwatupia vijana vitoa machozi, kwani kufanya hivyo ni kama kuwachochea kuzidi kujibu kwa kuwatupia mawe pia, na hivyo kuhatarisha hali nzima ya maandamano hayo ambapo baadhi wanaumia kwa kujeruhiwa, na pia vitoa machozi hivyo vinawaathiri kina mama hao na watoto wadogo katika nyumba zao.

Hata hivyo, inaarifiwa kwamba ombi la kina mama hao halikuonekana kuvua dafu kwani muda mfupi baadae vijana waliwatupia polisi mawe, na kuwafanya polisi pia kujibu kwa kutupa vitoa machozi wakiwatawanya vijana hao.

Kinara wa Azimio Raila Odinga aliitisha maandamano hayo kufanyika kila siku za Jumatatu na Alhamisi ili kushinikiza serikali ya Ruto kukubali matakwa yao.