Basi la abiria lapata ajali, lagonga ng'ombe 35 hadi kufa

Hata hivyo, haijulikani kama abiria ndani ya basi hilo walipata majeraha.

Muhtasari

• Kulingana na runinga ya Global TV Online kutoka nchini humo, haikujulikana ni abiria wangapi waliokuwemo ndani ya basi hilo na kama kuna abiria waliojeruhiwa.

Basi la abiria lagonga ng'ombe na kuua 35.
Basi la abiria lagonga ng'ombe na kuua 35.
Image: Screengrab

Ajali mbaya ya barabarani inayowahusisha mifugo imeripotiwa katika nchi jirani ya Tanzania ambapo basi la kampuni moja ya Zakaria Express linaripotiwa kupoteza mwelekeo na kuwagonga ng’ombe wapatao 35 hadi kufa.

Basi hilo ambalo lilikuwa linafanya safari zake kutoka mkoa wa Arusha Kaskazini wa taifa hilo kuelekea wilaya ya Kiteto.

Basi hilo liliwagonga makumi ya ng’ombe waliokuwa katika barabara hiyo na kuwaua 35 papo hapo huku wengine wane wakinusurika.

Kulingana na runinga ya Global TV Online kutoka nchini humo, haikujulikana ni abiria wangapi waliokuwemo ndani ya basi hilo na kama kuna abiria waliojeruhiwa.

Msururu wa ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikiripotiwa katika barabara nyingi umevutia sheria kali kuwekwa haswa nchini Kenya, haswa baada ya watu kadhaa kuripotiwa kufariki tangu mwezi Machi kwa ajali za barabarani.

Wiki jana baada ya matatu iliyokuwa imewabeba wanafunzi kupata ajali na kuuwa baadhi yao, waziri wa uchukuzi wa barabarani Kipchumba Murkomen alitoa maagizo mapya yakiwemo kupigwa marufuku kwa baadhi ya sacco ambazo zimekuwa magari yao yamekuwa yakihusika katika ajali za barabarani pamoja pia na marufuku kwa magari ya shule kufanya safari za usiku.

Mwezi Machi, basi la chuo kikuu cha Pwani lilipata ajali katika barabara ya Naivasha kuelekea Nakuru ambapo lilikuwa likiwasafirisha wanafunzi wa chuo hicho kwenda Eldoret kushiriki michezo ya vyuo vikuu.

Katika ajali hiyo, watu Zaidi ya 15 walipoteza maisha na makumi ya wengine wakisalia na majeraha mabaya.