Kwa nini 'Yesu wa Tongaren' anastahili kuchunguzwe - Gavana wa Bungoma, Lusaka

Akizungumza Jumamosi nyumbani kwake Kamukuywa, Lusaka alipuuzilia mbali Wekesa kwa kujifanya 'Yesu'.

Muhtasari

• Lusaka, hata hivyo, alimkana Yesu wa Tongaren akisema Bungoma imetoa watu wakuu wa Mungu ambao sasa wanatumikia taifa kuu la Kenya.

Lusaka ataka DCI kumchunguza Yesu wa Tongaren.
Lusaka ataka DCI kumchunguza Yesu wa Tongaren.
Image: Maktaba

Gavana wa Bungoma Ken Lusaka amemtaka Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) kumwita Eliud Wekesa almaarufu Yesu wa Tongaren baada ya mauaji ya Shakahola kaunti ya Kilifi.

Akizungumza Jumamosi nyumbani kwake Kamukuywa, Lusaka alipuuzilia mbali Wekesa kwa kujifanya 'Yesu' akibainisha kwamba anafaa kuitwa kujibu maswali ikiwa anahusishwa na imani za kidini kama Kasisi Paul Mackenzie wa Kilifi.

Mkuu huyo wa kaunti alikashifu mauaji hayo makubwa ya Shakahola akisema ni kinyume na mafundisho ya Mungu. Alitoa wito kwa wananchi kuwa makini na aina ya makanisa wanayohudhuria.

“Kama viongozi tulipokea tukio la Shakahola kwa mshtuko na simanzi, inasikitisha sana kwa sababu watu wengi wamepoteza mpendwa wao kutokana na vitendo vya ibada,” Lusaka alibainisha.

Lusaka, hata hivyo, alimkana Yesu wa Tongaren akisema Bungoma imetoa watu wakuu wa Mungu ambao sasa wanatumikia taifa kuu la Kenya.

"Bungoma ni nyumba ya watu wa Mungu kama vile Askofu Philip Anyolo, Askofu Eliud Wabukala, na Kadinali Otunga, kwa kutaja tu wachache, hatuwezi kuruhusu watu wachache kuchafua jina la Bungoma," alisema.

Viongozi wengine kutoka eneo hilo ambao wamemkosoa Yesu wa Tongaren wakitaka uchunguzi ufanyike haraka ni pamoja na Seneta wa Kakamega Bonnie Khalwale na mbunge wa Kimilili Didmus Barasa.

Lusaka alitoa wito kwa serikali kuendelea kuhangaisha na kuibua mauaji ya Shakahola yaliyosababishwa na ghiliba za kiroho zinazoongozwa na mazoea ya ibada.

“Mauaji ya Shakahola yamevuta hisia za nchi nzima na dunia kwa ujumla, kwa kweli inashangaza, vyombo vya uchunguzi viende kasi kulibaini hili na kuhakikisha waliopoteza wapendwa wao wanapata haki,” aliongeza Lusaka.