USHURU WA NYUMBA

Kiongozi aliyechanguliwa na 70% raia wa vibanda anapinga mpango wa kuwainua - Ruto

Mtu amechaguliwa na watu wake wanaoishi kwenye Slums, anapinga mpango huu - wazimu

Muhtasari

•Serikali tawala ya Kenya Kwanza, ilifanyia marekebisho mswada huo tata wa fedha, ambapo walishusha ushuru wa nyumba kutoka 3% hadi 1.5%.

• Kwanza nilikuwa naona tu juzi, mtu amechanguliwa, zaidi ya 70% waliomchagua wanaishi kwa slums, lakini anakataa huu mpango, si huyo ni mtu wazimu?

Image: RAIS RUTO// HISANI

Rais William Ruto ameshutumu vikali viongozi wanaopinga pendekezo lake kuhusu ushuru wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

Alipokuwa akiongoza hafla ya uzinduzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kerugoya, kaunti ya Kirinyaga, Ruto amewashutumu viongozi hao wanaopinga mswada wa fedha mwaka wa 2023, kile ambacho anakiita kuwa wazimu.

“Ulichaguliwa, ikaenda namna hii, ukapata kazi, ukapata cheo saa hii unaitwa mheshimiwa, mshahara yako, iko namna hiyo, iko sawa sawa. Lakini saa hii tukisema wacha tutoe kitu ili watu ambao walikuchagua nao wapate nyumba nzuri unaanza kiswahili.” Ruto alieleza.

Aliendelea na kusema kuwa, hata baadhi ya viongozi wanaopinga sera hiyo ya ushuru wa nyumba za bei nafuu waliiunga mkono wakati mmoja isipokuwa wakati huu wanataka kuipinga.“Wakenya walikuchagua juu upate hiyo kazi, si namna hiyo? Lazima pia nao wasaidie watoto wetu wapate ajira, au namna gani? Nikisema mpango huo huendelee wanaanza kiswahili, mnasema tulipe ushuru au tusilipe? Ili tuendeleze mpango wetu wa special economic zone? Watoto wetu wapate nafasi za ajira? au namna gani jameni?”

Rais Ruto aliendelea na kukiri kwamba, kuna kiongozi aliyemwona juzi ambaye alichaguliwa na zaidi ya kura 70% na raia wake bado wanaishi katika mitaa ya vibanda.“ Kwanza nilikuwa naona tu juzi, mtu amechanguliwa, zaidi ya 70% waliomchagua wanaishi kwa slums, lakini anakataa huu mpango, si huyo ni mtu wazimu?”

Serikali tawala ya Kenya Kwanza, ilifanyia marekebisho mswada huo tata wa fedha, ambapo walishusha ushuru wa nyumba kutoka 3% hadi 1.5%.

Haya yanajiri huku baadhi ya wakaazi kutoka eneo la mashariki mwa Nakuru wakirejelea mswada huo wa fedha 2023 kuwa “ Shakahola Finance Bill” Wakiwasuta vibaya watu ambao wanapendekeza mswada huo, na wale wanaopambana kukisambaratisha chama cha Jubilee. Watu hao pia wanakiri wataendelea kuushikilia vikali msimamo wao wa kuupinga mswada huo wa fedha.