Mvulana asimulia jinsi familia ilimtenga baada ya kumuoa msichana mwenye ugonjwa wa ngozi

Mvulana huyo alimkuta mrembo kanisani akiongoza kwaya na licha ya manundu usoni mwake, alijipata amevutiwa kwake na kuweka nadhiri ya kuwahi 'ndio' yake kwenye mapenzi.

Muhtasari

• Mara ya kwanza, msichana huyo alinikataa akifikiria kwamba 'nilikuwa nataka kulala tu naye kisha nimuache.'

• Baadaye alikubali lakini kwa sharti moja la kumtaka kuandamana naye kwenda mlimani kwa ajili ya kuombea uamuzi wake.

Mvulana asimulia kutengwa na familia baada ya kumuoa mrembo mwenye tatizo la ngozi.
Mvulana asimulia kutengwa na familia baada ya kumuoa mrembo mwenye tatizo la ngozi.
Image: YouTube//Screengrab

Mwanamume mmoja kutoka nchini Rwanda amewashangaza wengi kwa hadithi yake ya ajabu, jinsi alivyojipata kwenye mapenzi na mwanamke ambaye ana ugonjwa wa ngozi.

Nyindera Janvier alielezea kwamba alishindwa kuzuia mvuto wa mapenzi kutoka kwa Nyirantezimana Domitila, licha ya mrembo huo kuwa na uso wenye manundu na uliochubuka kwa chunusi kubwa na ndogo kutokana na matatizo ya ngozi.

Janvier akizungumza na chaneli moja ya mitandaoni alisema kuwa baada ya kumpenda mrembo huyo na kumuoa, alipoteza kuanzia marafiki, kazi na hata mitaji ya kumuingizia hela.

Janvier alisema kuwa mapenzi yake kwa mrembo Domitila yalianza miaka michache nyuma kanisani wakati aliingia kwenye ukumbi huo wa maombi na kumuona mrembo huyo ndiye alikuwa anaongoza kwaya kwa nyimbo.

Kipindi hicho Domitila alikuwa mlokole na hivyo Janvier alijikuta anampenda na hata kufanya udhubutu wa kumsogelea kwa ombi lake la kutaka wawe wapenzi, ombi ambalo hata hivyo lilipuuziliwa mbali na Domitila, msichana mlokole.

“Ni mimi ambaye nilimtongoza na alikataa kwa mara ya kwanza. Nilijaribu kumshawishi kuwa fikira zangu kwake zilikuwa chanya. Alinikataa akifikiria kwamba nilikuwa nataka kulala tu naye kisha nimuache. Lakini nilimuambia kwamba endapo angenikubali tungeanza familia pamoja, hivyo ndivyo aliona mimi si wa mchezo na mapenzi yetu yakaanza kunawiri,” Janvier alisema.

Kwa upande wake, Domitila alisema kuwa hakuitikia kwa kukurupuka bali alitafuta msaada wa maombi, na baada ya siku kadhaa alipata jibu la kuitikia ombi la Janvier.

“Wakati alikuja kwangu sikumuamini kwa sababu najua wavulana hudanganya wasichana. Kama mtu ambaye ni muombezi sana, najua wavulana ni waongo. Kwa hiyo nilimuambia aandamane name kwenda mlimani kwa maombi na alikubali,” alisema msichana huyo.

Kijana huyo baada ya kupokea jibu alilokuwa analisubiria kutoka kwa mpenzi wake, aliwaalika familia yake kukutana na mpenzi wake, na hapa ndipo alipata pigo la moyo.

“Ilikuwa ni jambo la busara kuwataarifu wazazi kuhusu nia yetu ya kuoana. Niliwaalika na walikubali. Lakini wakati waliona uso wake, walipigwa na butwaa kwa hali yake. Walijivuta nyuma mmoja baada ya mwingine na kuniambia kwamba uhusiano wangu na Domitila haungeruhusiwa kwendelea,” alikumbuka.

Mwanzoni kijana huyo alifikiria wazazi wake walikuwa wanamtania tu lakini kadri siku zilivyozidi kwenda, alijua walikuwa wanamaanisha kweli kuwa hawangeipa Baraka ndoa yake na Domitila.

“Nilijaribu kuwabadilisha mawazo yao nikiwaambia mimi nishapata chaguo langu kwa huyu mwanamke. Niliwasihi kumkubali kwa sababu ndiye mwanamke wangu wa pekee. Maombi yangu yote yalianguka kwenye masikio yaliyotiwa nta. Walirudi nyumbani wakiwa wamesawijika nyuso.”

“Walisambaza habari kuhusu uso ‘mbaya’ wa mpenzi wangu kwa marafiki zangu na hata kuwashauri wasihudhurie harusi yangu,” alisema kwa uchungu.

Alilazimika kuwakodi wanandoa tofauti kuwa mbadala ya wazazi wake siku ya harusi yake. Janvier alisema kuwa harusi yao ilikuwa ya fanaka mwisho wa siku lakini hata hivyo wazazi wake bado walimsakama kooni wakimtaka kumtaliki mke wake.

Lakini yeye alikuwa ameshairamba sumu ya penzi, na hata kwa maziwa asingeweza kupata tiba.