Gaza: Mtoto aokolewa akiwa hai kutoka tumboni mwa mama aliyeuawa katika shambulio la Israel

Mtoto huyo wa kike alisemekana kuwa na uzani wa 1.4kg na aliokolewa kupitia upasuaji wa dharura baada ya waokoaji kubaini kwamba mamake alifariki akiwa na ujauzito wa wiki 30. "Huruma zaidi ni kwamba alizaliwa akiwa yatima tayari!"

Muhtasari

• Vita baina ya jeshi la Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas katika ukanda wa Gaza vimeendelea tangu Oktoba mwaka jana.

• Usimamizi wa hospitali ya Rafah ulisema mtoto huyo atakuwa chini ya uangalizi maalum kwa kipindi cha wiki 3 hadi 4 kabla ya kuangalia mchakato wa kuondoka kwake.

Mwanamke mjamzito
Mwanamke mjamzito
Image: maktaba

Mtoto wa jinsia ya kike aliokolewa akiwa hai kutoka tumbo la mwanamke wa Palestina aliyeuawa katika shambulio la Israel kwenye ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, shambulio hilo lililotekelezwa usiku katika mji wa Rafah liliwaua raia wa Palestina wapatao 19.

Kati ya 19 hao, watoto 13 kutoka familia moja waliripotiwa kuangamia kwenye shambulio hilo.

Mtoto huyo wa kike alisemekana kuwa na uzani wa 1.4kg na aliokolewa kupitia upasuaji wa dharura baada ya waokoaji kubaini kwamba mamake alifariki akiwa na ujauzito wa wiki 30.

Usimamizi wa hospitali ya Rafah ulisema mtoto huyo atakuwa chini ya uangalizi maalum kwa kipindi cha wiki 3 hadi 4 kabla ya kuangalia mchakato wa kuondoka kwake.

“Baada ya kipindi hicho tutaangalia jinsi mtoto huyu ataondoka na atakwenda wapi, iwe kwa familia, kwa wajomba zake au hata babu na bibi. Hapa ndio kuna huruma Zaidi, hata kama mtoto huyo alisalimika, alizaliwa akiwa yatima tayari,” daktari alisema.

Vita baina ya jeshi la Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas katika ukanda wa Gaza vimeendelea tangu Oktoba mwaka jana.

Inaarifiwa kwamba Zaidi ya nusu ya wakaazi wa Gaza ambao ni takribani milioni 2.3 wametorokea katika mji wa Rafah kutafuta hifadhi dhidi ya mashambulizi ya jeshi la Israel.