BBI yataka makamishna wapya wa IEBC

BBI yapendekeza kuondoka kwa maafisa wa IEBC kabla ya uchaguzi wa 2022

Makamishna wa sasa watalazimika kuondoka

Muhtasari

 

  • BBI yataka makamishna wapya wa IEBC
  • Wasimamizi wa uchaguzi watasimamia tu uchaguzi mmoja mkuu

 Ripoti ya BBI imependekeza kwamba maafisa wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC waondoke afisini kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022

 Ripoti hiyo ilikabidhiwa rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga siku ya jumatano  huko Kisii .

 Kamati ilyotayarisha ripoti hiyo imependekeza kuajiriwa kwa makamishna wapya wa IEBC kabla ya uchaguzi mkuu ujao  ikisema hatua hiyo itaimarisha tume ya uchaguzi .

 Kamati hiyo imesema panafaa kuwa na  mwongozo wa wazi kuhusu majukumu  ya makamishna hao na wajibu wa tume mpya kusimamia uchaguzi mkuu .

  Kamati hiyo pia inapendekeza  kwamba wafanyikazi wa IEBC  waajiriwe kwa miakataba ya miaka mitatu  ambayo inaweza kuongezwa kwa mujibu wa utendakazi wao .

 Makamishna wa sasa wanaweza kusaidia katika utekelezaji  wa mageuzi yaliyopendekezwa  kwa kuweka mikakati ifaayo kwa matayarisho ya kuondoka afisini kwa hiari .

 Kamati hiyo pia inataka maafisa wanaosimamia uchaguzi kuteuliwa kutumia mfumo unaotumiwa wakati wa kuwaajiri  makamishna wa IEBC ikiwemo kuhusisha umma katika uteuzi wao

 Pia maafisa wa kusimaia uchaguzi hawataajiriwa kwa muda  na hawatasimamia zaidi ya uchaguzi mmoja

 Pia kamati hiyo imependekeza kwamba maafisa wakuu wa IEBC wahojiwe upya na  nyadhifa zao kubadilishwa ajina ili kuwa wakuu wa idara badala ya  wakurugenzi .