Nairobi: Sonko ataka mahakama kumzuia kaimu gavana Mutura kufanya teuzi

Muhtasari

  • Mutura anatarajiwa kuhudumu kwa siku 60.

  • Kaimu gavana siku ya Jumanne alitangaza mabadiliko katika baraza lake la mawaziri.

  • Sonko amewasilisha ya kupinga kutimuliwa kwake.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Gavana aliyetumuliwa afisini Mike Sonko Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko

Aliyekuwa gavana wa Nairobi aliyetimuliwa Mike Sonko amewasilisha kesi mahakamani akitaka agizo la kumzuia kaimu gavana Benson Mutura kufanya mabadiliko yoyote katika usimamizi wa kaunti hiyo hadi pale kesi aliyowalisha itakaposikizwa na kuamuliwa.

Mutura ambaye anatarajiwa kuhudumu katika wadhifa huo kwa kipindi cha miezi miwili siku ya Jumanne alitangaza mabadiliko katika baraza lake la mawaziri.  

Katika mabadiliko hayo Mutura alimrejesha aliyekuwa waziri wa elimu Janet Ouko na ambaye alijiuzulu mwaka 2019 baada ya kutofautiana na Gavana Sonko.

Mutura alimhamisha Lucia Mulwa kutoka wizara ya Elimu hadi Kilimo na kumteua Jairus Musumba kama Kaimu Katibu wa Kaunti. Alimteua pia Paul Mutungi kama Mkuu wa Wafanyikazi na Brian Weke kama mshauri wa sheria katika ofisi ya Gavana.

Sonko hata hivyo, katika ombi lililowasilishwa na wakili Harrison Kinyanjui siku ya Alhamisi, alisema Mutura hawezi kumteua tena Ouko kwa wadhifa huo kwa sababu alikuwa tayari kaondoka.

Tume ya uchaguzi na mipaka imelazimika kusitisha kwa muda mchakato wa kuandaa uchaguzi mdogo ili kujaza nafasi ya gavana wa Nairobi, baada ya Sonko kufanikiwa kupata agizo la mahakama kusitisha zoezi hilo.

Sonko amewasilisha kesi kupinga taratibi zilizofuatwa wakati alipotimuliwa na bunge la kaunti na kisha hoja hiyo kuungwa mkono na seneti.