Sekta ya hotel, kuna matumaini mwaka 2021

Muhtasari

  • Wadau katika sekta ya hoteli wanataka wahudumu katika sekta hiyo pia kuzingatiwa katika watu wa kwanza kupewa chanjo. 

  • Watalii wa ndani walipiga sana jeki sekta ya hoteli msimu wa sherehe.

  • Baadhi ya hoteli zilifungwa kutokana na  janga la corona na kufikia sasa hazijafunguliwa. 

Kwaheri 2020: Wafanyikazi na wageni katika Travelers Beach Hotel wakikata keki kuukaribisha mwaka 2021, Disemba 31, 2020.
Kwaheri 2020: Wafanyikazi na wageni katika Travelers Beach Hotel wakikata keki kuukaribisha mwaka 2021, Disemba 31, 2020.
Image: JOHN CHESOLI

TAARIFA YA BRIAN OTIENO

Wamiliki wa hoteli sasa wanategemea watalii wa ndani ya nchi kuwasaidia kusalia katika biashara kutokana na kutokuwepo kwa uhakika katika sekta hii kwa sababu ya janga la Covid-19.

Hata hivyo, kuwepo kwa chanjo ya Covid-19 kumeleta matumaini wamiliki wa hoteli sasa wana matumaini kuwa hali itaimarika.

Meneja mkurugenzi wa Travellers Beach Hotel Hillary Siele alisema mwaka wa 2020 ulikuwa mgumu zaidi na kwamba walijifunza mengi katika mazingira magumu.

 

Ana ujumbe kwa wamiliki wenzake wa hoteli na wadau wengine katika sekta hii - usifunge.

Hoteli zingine zilifungwa kwa muda mrefu na zingine hazijaweza kufungua hata baada ya vizuizi vilivyowekwa na serikali kuzuia kuenea kwa Covid-19 kulegezwa.

"Tuko katika safari yetu kupona," Siele aliiambia Star.

Alisema sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya ziliwapa matumaini wamiliki wengi wa hoteli kwani waliona idadi kubwa ya Wakenya ambayo hawajawahi kuona hapo nyuma.

"Wakenya wana matumaini na kuwepo kwao wakati wa msimu wa sherehe kulitupa nguvu na kutujaza matumaini," Siele alisema.

Meneja huyo mkurugenzi alisema kwamba walisajili mauzo mazuri na hali hii iliwapa changamoto kuweka juhudi zaidi katika kuimarisha huduma na bidhaa zinazolenga mahitaji ya watalii wa ndani.

Alitoa wito kwa serikali pia kuzingatia wamiliki wa hoteli kati ya watu wa kwanza kupewa chanjo ya Covid-19 mara tu chanjo hizo zitakapofika nchini.

Wafanyakazi wa afya na walimu watakuwa kati ya watu wa kwanza kupewa chanjo mara tu chanjo hizo zitakapofika nchini.

Kenya, kulingana na waziri wa Afya Mutahi Kagwe, itapokea shehena ya kwanza ya chanjo ya Covid-19 iliyotengenezwa na kampuni ya AstraZeneca wiki ya pili ya mwezi Februari. Serikali imeagiza dozi milioni 24.